AWESO AKABIDHI PIKIPIKI 216 KWA CBWSOs KUSAIDIA UHARAKISHAJI HUDUMA ZA MAJI VIJIJINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 22, 2026

AWESO AKABIDHI PIKIPIKI 216 KWA CBWSOs KUSAIDIA UHARAKISHAJI HUDUMA ZA MAJI VIJIJINI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma


Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, amezitaka Vyombo vya Utoaji wa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji bila vikwazo, ili kuona thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali pamoja na kutimiza adhma ya kumtua mama ndoo kichwani.

Aweso ametoa maelekezo hayo leo Januari 22, 2026 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki 216, seti 86 za vifaa vya kupima ubora wa maji na seti 128 za vifaa vinavyotumika katika uunganishaji na ukarabati wa mabomba ya maji ya ukubwa mbalimbali kwa CBWSOs.

Amesema licha ya Serikali kujenga miradi mingi ya maji, bado baadhi ya miradi hiyo haitoi huduma, huku sababu zinazotolewa zikiwa nyepesi na zisizokubalika kwa wananchi kukosa maji.

“Unakuta mradi wa zaidi ya shilingi bilioni tatu umejengwa lakini maji hayatoki. Ukiuliza unaambiwa LUKU hakuna au koki imeharibika. Hivi kweli LUKU inaisha wakati watendaji mpo? Hili si sawa. Jumuiya hizi za maji zifanye kazi kwa ufanisi ili kuleta tija iliyokusudiwa,” amesema Aweso.

Amefafanua kuwa Serikali haina mpango wa kuzifuta CBWSOs kwa kuwa zina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma, kwani ndizo zilizo karibu zaidi na wananchi, lakini amezitaka kuongeza ufanisi na uwajibikaji ili wananchi waone fahari ya kuwa na miradi ya maji iliyokamilika katika maeneo yao.

Aidha, Aweso amesema Wizara ya Maji imeanza mwaka 2026 kwa kufanya tathmini ya ndani ya watendaji wake wote ili kuongeza ufanisi katika sekta ya maji.

“Tutaendelea kuwatathmini hadi madereva, kwa sababu sekta ya maji inahitaji mchango wa kila mtumishi uonekane kwa vitendo. Mwananchi ukimhakikishia maji, kelele zinaisha,” ameongeza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka watoa huduma ya maji ngazi ya jamii kutumia lugha zenye staha kwa wananchi na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati, bila kusubiri kufikishwa ngazi za juu.

Akitoa maelezo ya kiufundi, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta S. Kirita, amesema Wizara ya Maji kupitia RUWASA imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji vijijini, lakini ujenzi wa miundombinu pekee hauwezi kutatua changamoto zote za sekta ndogo ya maji vijijini.

Amesema RUWASA imeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa makao makuu, mikoa, wilaya na CBWSOs, kwa lengo la kuhakikisha huduma ya maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira vijijini zinakuwa endelevu.

Kirita amesema kupitia Programu ya PforR kwa kutumia fedha za IPF, Wizara imefanikisha ununuzi wa pikipiki 216, seti 86 za vifaa vya kupima ubora wa maji na seti 128 za vifaa vya uunganishaji na ukarabati wa mabomba, vyenye thamani ya jumla ya shilingi 1,235,730,000 ikijumuisha VAT.

Ameeleza kuwa vifaa hivyo vinalenga kuboresha shughuli za uendeshaji na matengenezo (Operations and Maintenance) zinazofanywa na Ofisi za RUWASA wilaya pamoja na CBWSOs, ili kuhakikisha huduma ya maji na usafi wa mazingira vijijini inakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa Kirita, vifaa hivyo vitasambazwa katika mikoa 25, wilaya 128 na CBWSOs 88 nchini. Katika hafla hiyo, Waziri Aweso amekabidhi vifaa kwa wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma pamoja na CBWSOs tano ambazo ni Wilunze (Bahi), Farkwa (Chemba), Ntomoko Asilia (Kondoa), Panjole (Kongwa) na Muungano (Mpwapwa).








No comments:

Post a Comment