WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi,akizungumza wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi,akizungumza wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.


SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi, wakati akifungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange,akizungumza wakati wa Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa TANESCO lililofunguliwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Januari 22,2026 jijini Dodoma.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma
WAZIRI wa Nishati, Mhe. Deogratious Ndejembi, amesema matumizi ya mita janja (Smart Meters) ni miongoni mwa mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), yakilenga kuboresha huduma kwa wateja, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Akizungumza leo Januari 22, 2026 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa TANESCO, Waziri Ndejembi amelipongeza Shirika hilo kwa hatua kubwa za mageuzi, akisema mabadiliko yanayoendelea yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali na uongozi wa TANESCO katika kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.
Amesema pamoja na mita janja, TANESCO imeboresha mifumo ya mawasiliano kwa wateja kupitia matumizi ya WhatsApp Sogozi na Bulk SMS, hatua inayowezesha taarifa muhimu kuwafikia wananchi kwa wakati na kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima.
Aidha, Waziri amesema uzinduzi wa namba ya dharura 180 inayopigwa bila malipo umeleta urahisi mkubwa kwa wananchi kutoa malalamiko, kupata msaada wa haraka na kufuatilia huduma bila gharama.
Ameongeza kuwa mpango wa “Konekti Umeme – Pika kwa Umeme” kwa wateja na wafanyakazi ni miongoni mwa mageuzi muhimu yanayochochea matumizi sahihi ya umeme, kupunguza gharama za nishati kwa wananchi na kuongeza udhibiti wa mapato ya Shirika.
“Hatua hizi zinaonesha wazi kuwa TANESCO ipo katika mwelekeo sahihi wa kuboresha huduma, kupunguza upotevu wa mapato na kutatua kero za wananchi. Huu ni ushahidi wa nia njema ya uongozi wa Shirika,” amesema Waziri Ndejembi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha, wa uhakika na wa gharama nafuu, ili kutekeleza kikamilifu mkakati wa Serikali wa kuijenga Tanzania ya viwanda.
“Ili azma ya Serikali ifikiwe, ni lazima TANESCO ihakikishe uzalishaji wa umeme wa kutosha, miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme inaendelea kuboreshwa, na viwanda vinapata umeme wa uhakika wakati wote,” amesema.
Amefafanua kuwa hali hiyo itasaidia kuvutia wawekezaji wengi katika sekta ya viwanda na sekta nyingine, kuongeza ajira, kukuza uchumi wa Taifa na kutekeleza Mkakati wa Tanzania ya Viwanda kwa vitendo.
Waziri Ndejembi ameihakikishia TANESCO ushirikiano wa Serikali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme, ikiwemo miradi ya Gridi Imara na Nishati Jadidifu, kwa lengo la kuboresha zaidi upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amelishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia nyongeza ya mishahara na motisha kwa wafanyakazi, hatua aliyosema imeongeza utulivu na morali kwa wafanyakazi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Baraza Kuu la 55 la Wafanyakazi wa TANESCO linatarajiwa kujadili masuala ya kiutendaji, ustawi wa wafanyakazi pamoja na mikakati ya kuimarisha zaidi huduma za umeme kwa wananchi.

No comments:
Post a Comment