Imeelezwa kuwa ili kuhakikisha juhudi za kuwawezesha wanawake kupata fursa nyingi na nafasi katika fani mbalimbali ikiwemo uhandisi ni lazima kuunganisha nguvu kati Serikali na sekta binafsi nchini.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng. Bernard Kavishe wakati wa kusaini mkataba wa miaka mitatu na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wenye lengo la kuongeza usawa kazini na kukuza uwakilishi wa wanawake katika maamuzi ya uongozi chini ya program ijulikanayo kama Mwanamke wa Baadaye (FFP).
Makubaliano kati ya ERB na ATE chini ya Programu hiyo yamefanyika jijini Dar es Salaam.
“Idadi ndogo ya wahandisi wakike ni changamoto kwani katika malengo ya milenia na malengo endelevu ya dunia yanataka usawa kijinsia, hivyo kukosekana usawa ni dalili ya uduni wa maendeleo," amesema Mhandisi Kavishe.
Eng. Kavishe amesisitiza kuwa kupitia mradi wa mafunzo kwa wahandisi wahitimu (SEAP), yameendelea kutolewa na juhudi kubwa za kuhakikisha wahandisi wanawake wanapata fursa katika kujifunza kwa vitendo zinazoendelea.
Amebainisha kuwa chini ya mradi huo Serikali ya Tanzania imepata ufadhili kutoka Serikali ya Norway ambapo ufadhili huo ni wa miaka mitatu ambapo zaidi shilingi bilioni 4 zitatumika huku wahandisi wahitimu wa kike 100 wakitarajiwa kunufaika na mradi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba Doran amezishukuru taasisi na makampuni yanayoshiriki kama wadau katika program hii ambayo inatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika utendaji wa wanawake katika nafasi mbalimbali ikiwemo uongozi.
Mkataba huo baina ya ERB na ATE utasaidia kutoa mafunzo kwa wanawake 42 katika kipindi cha miaka mitatu na utagharimu zaidi ya shilingi milioni 90 za kitanzania huku ukitazamiwa kuongeza idadi kubwa ya wahandisi wa kike nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini ERB
No comments:
Post a Comment