RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI MATANKI YA MAFUTA KIGAMBONI, AAGIZA MRADI UKAMILIKE KWA WAKATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 3, 2026

RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI MATANKI YA MAFUTA KIGAMBONI, AAGIZA MRADI UKAMILIKE KWA WAKATI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo mahsusi kwa wizara na taasisi za Serikali kuhakikisha mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokelea na kuhifadhi mafuta katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, unatekelezwa kwa viwango vya kimataifa na kukamilika kwa wakati.


Akizungumza leo Machi 3, 2026, jijini Dar es Salaam mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa kimkakati katika Bandari ya Dar es Salaam, Rais Samia amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji kwa nchi za ukanda na kimataifa.

Ameiagiza Wizara ya Nishati kuimarisha miundombinu ya hifadhi ya mafuta na kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha kukabiliana na misukosuko ya bei katika soko la dunia.


Amesema kupanda kwa bei ya mafuta kimataifa ni changamoto inayoonyesha umuhimu wa kuwa na miundombinu madhubuti ya nishati.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa jiografia ya Tanzania inatoa fursa ya kipekee ya kuhudumia nchi zisizo na bandari, na kwamba Serikali imedhamiria kuitumia vyema fursa hiyo kwa maslahi ya taifa.


Amesema maboresho yanayoendelea katika sekta za bandari, reli na barabara yameongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa zaidi na kuongeza ushindani wake kimataifa. Amebainisha kuwa hatua hizo zimechangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa taifa.

Akizungumzia ushirikishwaji wa sekta binafsi, Rais Samia amesema uamuzi huo ulikuwa wa kimkakati na umeleta tija katika kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa bandari. Ameeleza kuwa fedha zilizookolewa zimeelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa matanki hayo ya mafuta.

Katika maelekezo yake, Rais ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia ubora, usalama wa mazingira na muda uliopangwa.

“Mradi huu umetumia fedha nyingi za Watanzania, hivyo lazima ujengwe kwa viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesisitiza Rais Samia.

Vilevile, ameitaka Wizara ya Nishati kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha mifumo ya uhakiki na ufuatiliaji wa shehena za mafuta kuanzia zinapowasili bandarini hadi zinaposambazwa, ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa na yenye uwazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, amemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uchukuzi na kuahidi kuwa wizara yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Mbassa, amesema dhumuni la mradi huo ni kuongeza uwezo wa nchi kupokea na kuhudumia shehena za mafuta kwa ufanisi zaidi, sambamba na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Rais Samia amehitimisha kwa kuwataka wakandarasi na washauri wa mradi kuhakikisha wanatekeleza kazi kwa uadilifu, ubora na kwa wakati ili kuwezesha mradi huo kuanza kufanya kazi mapema mwaka ujao, akieleza matumaini yake kuwa utachangia kukuza biashara, ajira na mapato ya taifa.

No comments:

Post a Comment