TEKNOLOJIA SI TISHIO, NI FURSA KWA VIJANA WENYE UJUZI – SANGU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 3, 2026

TEKNOLOJIA SI TISHIO, NI FURSA KWA VIJANA WENYE UJUZI – SANGU




Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema teknolojia si tishio kwa kijana aliye na ujuzi na maadili bali ni fursa kwa aliye tayari kujifunza na kubadilika.

Amesema kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunahitaji nguvukazi mahiri yenye uwezo wa kuhimili mabadiliko na kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.

Waziri Sangu ameyasema hayo Machi 3, 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi awamu ya nane kwa mwaka 2025/2026 uliofanyika katika Chuo cha Ufundi cha Don Bosco Vocational Training Centre Dodoma, ambapo alizitaka taasisi zilizopata nafasi kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Amewataka vijana kutumia fursa wanazozipata kuonesha uwezo wao ili waweze kujiajiri, kuajiriwa na hata kuajiri vijana wenzao katika kipindi hiki cha mapinduzi ya teknolojia.

Amesema vijana wanapaswa kuelewa na kuitumia akili unde (Artificial Intelligence – AI), akisisitiza kuwa si jambo la baadaye bali ni sehemu ya sasa ya mazingira ya kazi. Ameongeza kuwa mafunzo wanayopata lazima yaendane na maendeleo ya sasa ya TEHAMA na matumizi ya mifumo ya kidigitali.

Katika hatua nyingine, amesema kuwa ndani ya miezi mitatu zaidi ya vijana 5,000 wamepata fursa za ajira nje ya nchi, huku vijana 1,150 wakitarajiwa kuondoka hivi karibuni kufanya kazi katika kada mbalimbali ikiwemo udereva na ufundi mitambo.

 Ameongeza kuwa Serikali inalenga kuona zaidi ya vijana 6,000 wanapata ajira nje ya nchi katika kipindi hicho.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeanzisha programu maalum ya kuongeza ujuzi kwa nguvukazi hususan wenye ujuzi wa chini ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa. Lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 taifa linakuwa na nguvukazi yenye ujuzi unaoakisi uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu unaoongozwa na maarifa na maendeleo ya viwanda.

Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano inaendelea kutekeleza programu ya kukuza ujuzi kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Ameongeza kuwa Serikali imewezesha vijana 5,706 kupitia vyuo sita vilivyokidhi vigezo, ambapo kati yao wanaume ni 3,355 na wanawake 2,351. Jumla ya Shilingi bilioni 4.3 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo.

Vilevile, amesema wanagenzi 480 kutoka Mkoa wa Dodoma wamepata ufadhili wa asilimia 100 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuwataka washiriki kuonesha nidhamu, bidii, ubunifu na uadilifu ili mafanikio yao yawe chachu ya maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Zuhura Yunus amesema lengo la uzinduzi huo ni kutangaza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, kuhamasisha vijana kushiriki mafunzo na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kukuza ajira na uchumi.

Amebainisha kuwa programu hiyo ilianza mwaka 2016/2017 kwa lengo la kuongeza ujuzi wa nguvukazi katika soko la ajira, na hadi Februari 2026 jumla ya wanufaika 168,657 wamenufaika.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Don Bosco Vocational Training Centre Dodoma, Mhandisi Dkt. Justin Mulebya, amesema chuo hicho hutoa mafunzo ya ufundi stadi na ufundi sanifu kuanzia ngazi ya 1 hadi ngazi ya 6 (Diploma). Ameongeza kuwa mwaka 2026 chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 650, ambapo wanagenzi 235 wanafadhiliwa na Serikali, wakiwemo wasichana 74 (31.5%) na wavulana 161 (68.5%).








No comments:

Post a Comment