JESHI LA POLISI LAWEKA MIKAKATI KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA NA UCHAGUZI MKUU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 28, 2024

JESHI LA POLISI LAWEKA MIKAKATI KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA NA UCHAGUZI MKUU


Na, Okuly Julius-Dodoma 


JESHI la Polisi Nchini limewahakikishia Watanzania kuwa limeweka mikakati ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu.


Hayo yameelezwa na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi David Misime leo Machi 28,2024 jijini Dodoma ,wakati akiwasilisha mada kuhusu usalama wa wananchi wakiwemo waandishi wa habari katika kuelekea kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa ana uchaguzi mkuu mwakani.


Ametaja mikakati mingine kuwa ni kujenga mahusiano mazuri kati ya jeshi la polisi na na kuendelea kusimamia sheria zinazotakiwa.


“Jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu katika kuzingatia hilo kuna mikakati ambayo tumejiwekea ikiwemo kutoa elimu kwa askari polisi, wananchi na waandishi wa habari ili kila mtu ajue wajibu wake,”alisema


Ameongeza kuwa: ”Siku ya uchaguzi jeshi la polisi litahakikisha linalinda vifaa vya uchaguzi na kuhakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama na kuhakikisha hakuna anayefanya kampeni siku ya uchaguzi ili kuzuia vurugu,”



Kuhusu wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi Misime alisema jeshi la polisi litahakikisha linadhibiti vurugu na uvunjifu wa amani.


Kwa upande wake Rais wa Muunganiko wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Deogratius Nsonkolo aliishukuru serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazingira sahihi na bora kwa waandishi wa Habari kufanya kazi.


Amesema lengo la kuandaa mdahalo huo ni kushirikiana na wadau kuona ni namna gani ya kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wa Habari hususan katika kipindi kuelekea uchaguzi.


“Tunaipongeza serikali ya Awamu ya sita kwa kuboresha mazingira safi kwa waandishi wa Habari. Hivi sasa waandishi wanafanya kazi kwa utulivu na katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu tunaamini mazingira yatakuwa bora Zaidi,”alieleza


Naye Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Dk.Rose Reuben alisema katika kuelekea uchaguzi wandishi wa Habari kuzingatia maadili.


“Wandishi wa Habari zingatieni sana maadili hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi hakikisha taarifa unayotoa umejiridhisha na imetoka katika vyanzo vinavyotambulika ili kuondoa utata ambao unaweza kutokea baada ya kutoa taarifa za uongo,”alisisitiza


Awali mmoja wa washiriki wa Mdahalo huo Ronald Sonyo alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari hasa katika kipindi hiki tunapoelekea katika uchaguzi.


“Tunashukuru UTPC kwa kuwezesha mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka na tunaamini yatasaidia sana waandishi kufanya kazi kwa utaratibu ili kuzuia misuguano ambayo inaweza kutokea wakati wakitekeleza majukumu yao,”alieleza


No comments:

Post a Comment