WIZARA YA ULINZI YAJIVUNIA MCHANGO WAKE KATIKA UJENZI WA UCHUMI IMARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 3, 2024

WIZARA YA ULINZI YAJIVUNIA MCHANGO WAKE KATIKA UJENZI WA UCHUMI IMARA


Na Okuly Julius - Dodoma

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Dkt. Stergomena Tax amesema Wizara hiyo kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu ambapo yote hayo yamewezekana kutokana na kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mipango madhubuti katika ulinzi wa nchi.

Dkt.Tax ameyasema hayo leo Aprili 3, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya miaka 60 ya muungano.

Amesema wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa ni miongoni mwa wizara zinazotekeleza masuala ya muungano na jukumu la kuandaa sera ya taifa ya ulinzi na kusimamia utekelezaji wake.


“Tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Ulinzi na JKT inayo kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu zote sita (6) za uongozi, Awamu ya kwanza ilijenga nchi, umoja wa kitaifa, iliunda Jeshi, iliandaa vijana kwa ulinzi wa nchi yao ambao walimshinda Nduli Iddi Amin Dada, mafanikio haya yameendelezwa na awamu zilizofuata zote,” amesema Mhe. Tax.


Amesema Serikali kupitia wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa wanajeshi na watumishi wa umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu kwa kuwapatia makazi bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali ikiwa kupandisha vyeo kulingana vigezo na taratibu.

Mhe Tax amesema,“Hadi sasa serikali imejenga nyumba za makazi katika kambi mbalimbali za jeshi kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Mwanza, Pemba, Pwani, Rukwa, Tabora, na Tanga. Aidha, ujenzi wa nyumba hizo, kwa kiasi kikubwa umepunguza uhaba wa nyumba pamoja na changamoto zitokanazo na wanajeshi kuishi uraiani”.

Amesema wizara imefanikiwa pia kwenye utoaji wa
huduma za afya na tiba kupitia hospitali za jeshi za kanda ambazo ni Lugalo Dar es Salaam, MH Mwanza, Bububu Zanzibar, Mirambo Tabora, MH Arusha, MH Mbeya ambazo hutoa huduma kwa wanajeshi pamoja na wananchi waishio maeneo yaliyo jirani na kambi za jeshi huku takwimu zikionesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanaopata huduma katika hospitali za jeshi ni raia wasiyo wanajeshi.

Pia Mhe Tax amesema kwa upande wa michezo katika kipindi cha miaka 60 ya muungano imefanya vizuri ambapo timu za majeshi yaliyo chini ya wizara ya ulinzi na JKT zimefanikiwa, ikiwemo timu ya mashujaa FC iliyopo Kigoma iliyofanikiwa kupanda ligi kuu Tanzania bara kuungana na timu ya JKT Tanzania. Huku timu ya wanawake ya mpira wa miguu ya JKT Queens nayo imeendelea kufanya vizuri katika michezo ya ligi kuu ya wanawake na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa CECAFA kwa mwaka 2022/2023 iliyowapa tiketi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika kwa wanawake nchini Ivory Coast.

Mhe. Tax ameeleza kuwa serikali kupitia wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa, imeendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa, kikanda na nchi rafiki kutekeleza diplomasia ya ulinzi.

Pia, amesema kupitia SUMAJKT imekuwa ikichangia katika pato la taifa kupitia uzalishaji mali na kulipa kodi stahiki kupitia kampuni zake tanzu na miradi mbalimbali na kufanikiwa pia kuongeza ajira takribani 36,479 (29,758 ajira rasmi, na 6720 ajira zisizo rasmi) kwa vijana wa kitanzania kupitia kampuni zake tanzu, viwanda, na miradi mbalimbali.

Awali Mhe. Tax ameeleza dira ya wizara Ulinzi na jeshi la kujenga taifa kuwa ni, "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye Amani na Usalama" na dhima yake ni"kulinda mamlaka, mipaka ya nchi na maslahi ya taifa kwa kutekeleza sera ya ulinzi wa taifa katika kudumisha amani na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment