Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewatembelea Mabalozi wa Tanzania wanaoshiriki warsha ya siku 4 ambayo imekamilika mjini Kibaha leo Aprili 24, 2024 kwa kufikia makubaliano mbalimbali ambayo yanalenga kuipaisha diplomasia ya Tanzania duniani.
Dkt. Nchimbi aliwapongeza Mabalozi hao kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuitangaza nchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la biashara, uwekezaji na utalii nchini.
Warsha hiyo ambayo ililazimika kumalizika usiku kila siku ilifanyika chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) ilijadili mikakati ya kuboresha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na namna ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ambazo zimekuwa kikwazo kufikia ufanisi wa shughuli za Wizara hiyo.
Katika siku zao 4, Mabalozi pamoja na mambo mengine, walipitia mikakati ya Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, Uendelezaji wa majengo ya ofisi na makazi ya Balozi, Diplomasia ya Umma na Diplomasia ya kidigitali na viashiria vya kupima utendaji (Key Performance Indicators- KPIs).
Mabalozi walieleza kuwa kukamilika kwa nyaraka hizo ambazo hazikuwahi kuwepo Wizarani kabla ni chachu katika mwelekeo mpya wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Mabalozi walisisitiza umuhimu wa kumaliza changamoto za kimawasiliano baina yao na wadau ambazo zimekuwa kikwazo za kukamilika kwa wakati kwa fursa na miradi ambayo imekuwa ikiletwa nchini. Changamoto nyingine kubwa ambayo Mabalozi wamesisitiza itafutiwe ufumbuzi ni uwezo mdogo wa nchi yetu wa kuzalisha bidhaa za kukidhi soko katika maeneo yao ya uwakilishi.
Waheshimiwa Mabalozi walisema kuna soko kubwa la nyama, maparachichi, korosho, mchele na bidhaa nyingine lakini hakuna bidhaa za kutosha nchini za kulisha soko hilo.
Mabalozi katika warsha hiyo walipata fursa ya kusikiliza nasaha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa njia ya mtandao ambaye aliwataka kuwa jicho la Tanzania katika maeneo yao ya uwakilishi ili nchi isipitwe na mabadiliko yanayotokea duniani.
Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka alifika katika warsha hiyo na kuwambia Mabalozi kuwa wapo katika Wizara iliyokusanya watu wenye taaluma, ujuzi, uzoefu na historia ya kutoka sekta tofauti mchini. Aliwasihi washirikiane kutumia fursa hiyo kuharakisha mabadiliko ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na kutatua changamoto zinazowakabili.
Taasisi kadhaa pia zilialikwa na kuwasilisha mada kuhusu shughuli za ofisi zao ambazo ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Benki ya Azania.
Warsha hiyo pia wakati wa ufunguzi, walikaribishwa Mabalozi wastaafu ambao walipata fursa ya kubadilishana uzoefu na Mabalozi wa sasa kwa lengo moja tu la kujengeana uwezo wa kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na mataifa mengine, mashirika ya Kikanda na Kimataifa.
Waziri Makamba ambaye ana muda wa takribani miezi 7 tokea ahamishiwe Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema Wizara inaweza kufanya zaidi kuliko inavyofanya hivi sasa. Hivyo, warsha hiyo iliandaliwa ili kupigana msasa wa kufikia nchi ya ahadi.
No comments:
Post a Comment