Serikali imesema hadi kufikia Mwezi, Machi 2024 jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishiwa huduma ya umeme.
Hayo yamesema na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko Bungeni, leo Tarehe 24 Aprili, 2024, Jijini Dodoma wakati akisoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi vijijini, jumla ya taasisi 63,509 zinazotoa huduma kwa jamii ikiwemo ya elimu, biashara, pampu za maji, vituo vya afya na nyumba za ibada zilikuwa zimeunganishiwa umeme, ikilinganishwa na taasisi 43,925 Mwezi Aprili, 2023.
Vilevile, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kupeleka umeme vitongojini na katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, viwanda na kilimo, katika shule pamoja na mahakama za mwanzo vijijini.
Dkt. Biteko amesema katika mwaka 2024/25, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kupeleka nishati vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo. Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ununuzi wa wakandarasi wa kutekeleza mradi, kufanya usanifu wa kina wa mradi na kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi.
Miradi mingine ambayo itapewa kipaumbele ni pamoja na Mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 3,060 (vitongoji 15 kila Jimbo) kwa kujenga miundombinu ya mradi, kufunga transfoma na kuunganisha wateja.
Miradi mingine, itakayotekelezwa ni mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili (B); Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili (C); Mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Vijijini-Miji; (PERI Urban); Mradi wa kusambaza umeme katika Migodi Midogo, Maeneo ya Kilimo na Viwanda; Mradi wa kupeleka umeme katika minara ya mawasiliano ya simu na mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua kwenye makazi yaliyopo Visiwani na yaliyopo mbali na Gridi ya Taifa.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau, itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 kwa kupatia ufumbuzi vikwazo vya matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo gharama kubwa, upatikanaji hafifu na uhaba wa miundombinu yake na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.
Aidha, Mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye Kaya zilizopo katika maeneo ya Vijijini na Vijiji-Miji; kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya ununuzi wa mashine zitakazotumika katika uzalishaji wa mkaa huo; kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ujenzi wa miundombinu ya nishati ya kupikia katika maeneo 211 pamoja na kuendelea na usambazaji wa gesi asilia majumbani, hususan katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.
No comments:
Post a Comment