MAAFISA TARAFA NA WATENDAJI KATA WAPIGWA MSASA UTAWALA BORA, UKUSANYAJI WA MAPATO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, April 28, 2024

MAAFISA TARAFA NA WATENDAJI KATA WAPIGWA MSASA UTAWALA BORA, UKUSANYAJI WA MAPATO


Na OR - TAMISEMI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Bw. Mohamed Gombati amewaeleza Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kuwa mafunzo watakayopatiwa yatasaidie kuwaongezea ujuzi na maarifa katika kutekeleza majukumu yao na kupunguza au kuondoa changamoto zilizopo katika kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao.

Bw. Gombati ameyasema hayo Aprili 27, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata Mkoani Geita yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Bw. Gombati amesema changamoto ambazo zinaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi ya kata na tarafa nyingi zinatokana na kutokuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika utendaji kazi wa kila siku kwa Maafisa hao.

Amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kwenda kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitatua na kuhakikisha taarifa zake zinachukuliwa hatua na zinawekwa katika maandishi ili kutunza kumbukumbu pamoja na kuziwasilisha kwa Wakurungenzi wao wa Halmashauri kwa ajili ya utatuzi.

Pia amewataka kuendelea kutengeneza mipango kazi ya kutembelea katika Tarafa, Kata, Vijiji ili kuweza kutambua kero zilizopo na kutoa ushauri kwa Wakurugenzi wao kuhusiana na kero zinazojitokeza na si kusubiri mpaka viongozi wakubwa kwenda kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Aidha, amewaasa kujadili kuhusu taarifa za mapato na matumizi huku akiwaeleza kuwa kwa sasa hali ya makusanyo ya mapato kwenye Halmashauri zao sio mazuri na kwamba waongeze nguvu katika kukusanya mapato pamoja na kuwa wabunifu katika kubuni vyanzo vya mapato na kuviwasilisha kwenye Mamlaka zao ili kuongeza mapato.

" ni matumaini yangu kupitia mafunzo haya mtakusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kufikia malengo ambayo Halmashauri imejiwekea" alisema Bw. Gombati"

No comments:

Post a Comment