Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inaendelea na urejeshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja ambayo imeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha na kuleta athari katika baadhi ya maeneo Mkoani Dar es Salaam ikiwemo barabara ya Chanika - Ukonga.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Nimpha Peter ameeleza kuwa mvua zilizokuwa zikinyesha katika Mkoa huo zimesababisha maji kupita juu katika eneo ya Kinyamwezi 3, barabara ya Chanika - Ukonga na kusababisha mmomonyoko katika kingo za barabara na baadhi ya makalvati.
“Hatua za awali, tumeleta mawe na kuyajaza katika maeneo yenye mmomonyoko pamoja na kurudishia makalvati katika hali yake na kazi zingine zitakazoendelea ni kuweka zege pamoja na kujenga mitaro ya maji iliyoharibika”, amesema Mhandisi Nimpha.
Amefafanua kuwa hivi sasa wananchi wameruhusiwa kupita katika eneo hilo upande mmoja na wakikamilisha matengenezo wataruhusu pande zote mbili.
Aidha, Mhandisi Nimpha amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakati wanapopita katika barabara ya Chanika - Ukonga pindi wanapoendelea kufanya matengenezo maeneo yote yaliyopata athari.
kwa upande wake, Mkandarasi wa Kampuni ya Goodpromise Mhandisi Rueben Kitutu ameeleza kuwa kazi zinazoendelea kufanyika katika eneo la Kinyamwezi 3 ni kurekebisha sehemu zote zilizoharibiwa na mvua pamoja na kuongeza upana wa malvati ili kuruhusu maji yaweze kupita kwa urahisi.
Naye, Mkazi wa Chanika, Bw. Hamis Mirambo ameishukuru Serikali kwa jitihada za maboresho ya barabara ya Chanika hadi Ukonga kwa kuwa siku mbili za nyuma hali ilikuwa mbaya lakini kwa sasa hali ni nzuri na wakazi wa maeneo haya wanaendelea na shughuli zao za kila siku.
Pia, Mkazi wa Kipawa Bi. Neema Lema ameiomba Serikali kufanya matengenezo ya kudumu katika barabara ya Chanika-Ukonga kwani kwa muda wa wiki mbili maji yamekuwa yakipita juu ya barabara na wananchi wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya kuvuka pamoja na kukuaa foleni kwa muda mrefu hivyo ameomba kuharakisha matengenezo ili barabar hiyo isiweze kuleta madhara kwa jamii inayoizunguka.
No comments:
Post a Comment