MGOMO WA MADAKTARI KENYA: UMMA ULIVYOBAKI NJIA PANDA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 16, 2024

MGOMO WA MADAKTARI KENYA: UMMA ULIVYOBAKI NJIA PANDA.


Vitanda vingi katika wadi ya wazazi ya Hospitali ya Kihara Level 4 nje kidogo ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi, havina watu.


Ni tatu tu ambazo zilizo na watu kati ya zaidi ya dazeni.


Muuguzi mmoja anasema hospitali hiyo haiwapokei wanawake wanaohitaji upasuaji kwa vile hakuna daktari wa kuwafanyia upasuaji huo.


Madaktari wa hapa na kote nchini wamekuwa kwenye mgomo kwa takribani mwezi mmoja sasa.


Hospitali za umma ni karibu tupu. Kuna ukimya katika maeneo ambayo kwa kawaida yamejaa watu wanaotafuta huduma nyingi muhimu.


Wagonjwa sasa wanalazimika kwenda katika hospitali za binafsi za gharama kubwa au kuchelewesha matibabu, na kusababisha magonjwa sugu na wakati mwingine vifo.


Madaktari wanagoma wakidai masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na malipo na kushindwa kuajiri madaktari waliofunzwa, ambao hawawezi kufuzu bila kupata nafasi ya mafunzo.


Madaktari wanafahamu matatizo yanayosababishwa na mgomo huo lakini wanadai kuwa kuchukua hatua ni muhimu "ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya" kwa muda mrefu, kwani mazingira yao ya kazi na ukosefu wa vifaa vinamaanisha hawawezi kutibu wagonjwa ipasavyo, anasema. Davji Bhimji, katibu mkuu wa chama cha madaktari, KMPDU.


"Wakati mwingine tuko tu kusimamia kifo," anaambia BBC.





Rais William Ruto amewataka madaktari wanaogoma kurejea kazini na kukubaliana na kiwango ambacho serikali imetoa akisema ni lazima nchi “iishi kulingana na uwezo wetu”.


Wengi ambao wamelazimika kutegemea huduma ya afya ya umma wanatia huruma kwani wamejionea matatizo wenyewe.


Mwanamke mmoja anaiambia BBC kwamba shemeji yake, ambaye alikuwa katika maumivu na alihitaji kufanyiwa upasuaji, alimpoteza mtoto wake ambaye alikuwa tumboni kwa sababu ya mgomo huo.


Mgonjwa huyo alikuwa amesafiri kutoka magharibi mwa Kenya, ambako hakuweza kupata matibabu, hadi katika hospitali kuu ya rufaa jijini Nairobi, lakini alikataliwa.


Hatimaye alipelekwa katika hospitali binafsi lakini alikuwa amechelewa kumuokoa mtoto wake.


Lucy Bright Mbugua, 26, anasema mtoto wake wa miezi 10 amekuwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi tangu Januari.


Mtoto wake yuko katika hali inayohitaji uangalizi wa mara kwa mara lakini ni madaktari wachache tu wanaopatikana. Sasa wanakuja karibu mara mbili kwa wiki badala ya kila siku.


"Inauma wakati hakuna huduma. Mtoto anateseka na hakuna dawa," aliiambia BBC.


Mama yake, Anne, anasema mara nyingi hukaa usiku katika kituo cha wagonjwa wa nje ili awe karibu na binti yake, na kuokoa gharama za usafiri.


Mkulima huyo mdogo, ambaye alikuja Nairobi kutoka nyumbani kwake kijijini umbali wa kilomita 200 (maili 125) baada ya mjukuu wake kuugua, anasema anajaribu kumsaidia bintiye kifedha lakini ni vigumu sana.


"Kwa nini hawawezi kukaa chini na kukubaliana," anasema juu ya madaktari wanaogoma na serikali, akiongeza kuwa "sisi, samaki wadogo, tunateseka sana", maoni yaliyoungwa mkono na wengi.





Wengine wamekuwa wakitafuta kitulizo katika maombi.


Mchungaji mmoja huko Kibera, mojawapo ya makazi duni makubwa jijini Nairobi, anasema amekuwa akiwaona wagonjwa watano kwa wiki.


"Unajua kwamba wanahitaji kuonwa na madaktari, lakini ikiwa hakuna matibabu, unatoa maombi ili waache kuwa na mawazo mengine au kukata tamaa," Mchungaji Stephen Genda anaambia BBC.

Matatizo hayo sasa yameongezeka huku maafisa wa kliniki wakijiunga na mgomo huo.


Wanatoa huduma kwa wagonjwa wa nje na ni uti wa mgongo wa huduma ya afya, hasa katika maeneo ya vijijini. Lakini wameapa kutotetereka hadi matakwa yao yatimizwe.


"Serikali haitatoa chochote bila vita," anasema Peterson Wachira, mwenyekiti wa Muungano wa Maafisa wa Kliniki nchini Kenya.


Serikali inasema inalipa malimbikizo ya mishahara kwa madaktari na imejitolea kuajiri madaktari waliohitimu.


Hiyo ilifuatia mazungumzo, ikiwa ni pamoja na mazungumzo yaliyoidhinishwa na mahakama ambayo yalihusisha wawakilishi wa idara tofauti za serikali.


Lakini madaktari waliikataa, wakisema malipo yaliyokuwa yakitolewa kwa wahitimu yalifikia punguzo kubwa la kiasi kilichokubaliwa katika mkataba wa 2017.


Serikali iliweka idadi hiyo mpya kuwa $540 (£430) kwa mwezi, lakini muungano huo unasema $1,600 zilikuwa zimekubaliwa kwa malipo na marupurupu katika mpango huo.


Mamlaka hazijaweza kuajiri madaktari wote waliofunzwa kwani wanasema hakuna pesa za kutosha kuwalipa wahitimu wote wanaotarajiwa.

Hili limewaacha wengi wakiwa na uchungu na kujihisi wasiotakiwa.





Micheni Mike, daktari aliyehitimu anayesubiri kupelekwa kwenye kituo cha kazi, aliiambia BBC mwanzoni mwa mgomo kwamba serikali "haiwapi kipaumbele na ujuzi ulionao".


Shirley Ogalo, daktari wa upasuaji wa meno ambaye pia anasubiri kuajiriwa, anasema kuwa kuhitimu ilikuwa wakati mzuri sana "lakini sasa ninapigana".


"Unaona wenzako, watu waliofanya kozi nyingine, wananawiri. Wengine wameanzisha familia. Inasikitisha, inafadhaisha sana," anaiambia BBC.

Mamlaka zinaanza kuchukua mkondo mgumu zaidi.


Baadhi ya magavana wanaoongoza serikali za kaunti zinazohusika na shughuli nyingi za afya wametishia kuwafuta kazi madaktari hao.


Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Magavana, Muthomi Njuki, amesema baadhi ya matakwa ya madaktari hayakuwa ya busara na ni magumu kuyatekeleza.


Hospitali moja ya umma jijini Nairobi ilitangaza wiki jana kuwa inawaachisha kazi zaidi ya madaktari 100 walioshiriki mgomo huo. Lakini hadi sasa wafanyakazi wa afya wameapa kushikilia msimamo wao.


Bw Bhimji alishutumu serikali kwa "kutojali kuhusu huduma tunazotoa, la sivyo kama wangekuwa na wasiwasi wangekaa chini na kujadili" masuala hayo.


Viongozi wa kidini na viongozi wa upinzani ni miongoni mwa waliotoa wito kwa serikali kuanzisha upya mazungumzo na madaktari na hospitali hizo zirudishe huduma.


Lakini hii bado inaweza kuendelea kwa miezi, kusimamishwa mnamo 2017 kulidumu kama siku 100.


Lakini Bi Mbugua, ambaye ana mtoto mchanga mwenye umri wa miezi 10 ambaye ni mgonjwa, anatumai mgomo huo utakwisha hivi karibuni.

"Tunataka madaktari warudi ili mambo yawe ya kawaida tena," anasema.

No comments:

Post a Comment