
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi chake cha pili ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali ataendelea kuimarisha na kuunganisha miundombinu ya usafiri ikiwemo bandari, reli, viwanja vya ndege, barabara na madaraja ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kote nchini.
Dkt. Samia ambaye anatarajiwa kuhitimisha kampeni zake mwanzoni mwa Wiki ijayo Mkoani Mwanza, tayari kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 anasema jitihada hizo zitaenda sambamba na uboreshaji wa mifumo ya uagizaji na utoaji wa mizigo nchini, kipaumbele kikiwa ni ujenzi wa madaraja yanayoelekea katika maeneo yanayochochea shughuli za kiuchumi na huduma za jamii.
Miongoni mwake ni pamoja na kukamilisha kwa kiwango cha lami ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha Makao makuu ya Mikoa yote nchini na zile zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na kufanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa barabara za Dar Es Salaam- Kibiti- Lindi- Mingoyo (Km16).
Barabara nyingine iliyoahidiwa kutekelezwa na Chama Cha Mapinduzi CCM ni ya Dar Es Salaam- Morogoro- Dodoma- Singida- Shinyanga- Mwanza (Km477), Barabara ya TANZAM, (Tumbatu Jct- Mangae/Melela- Mikumi- Iyovi (Km158.45), barabara ya Dar Es Salaam- Chalinze- Segera- Arusha (Km648) na kuanza jwa ujenzi wa barabara za juu (Flyover) katika Makutano ya Morocco, Mwenge, Magomeni na Tabata Jijini Dar Es Salaam.
Dkt. Samia, aliyeweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuaminiwa na kupitishwa na Chama chake kuwania nafasi ya Urais wa Tanzania, kadhalika ameahidi kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika Miji na Majiji ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Babati, Singida, Songea na Iringa na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi katika barabara za Ali Hassan Mwinyi- Morocco- Mwenge- Tegeta na Mandela.
Dkt. Samia kadhalika ameahidi kujenga reli na kuweka usafiri wa treni za Mijini (Metro) katika Majiji ya Dar Es Salaam n Dodoma ili kupunguza msongamano na kurahisisha usafiri, kuanza ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganisha bandari ya Tanga kuelekea Arusha hadi Musoma (Km1,108), reli inayotazamiwa kuunganishwa na reli ya SGR kutoka Dar Es Salaam hadi Kigoma.

No comments:
Post a Comment