SERIKALI YATENGA BILIONI 5.2 UJENZI WA MIUNDOMBINU MBINGA: DC MAKORI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 25, 2025

SERIKALI YATENGA BILIONI 5.2 UJENZI WA MIUNDOMBINU MBINGA: DC MAKORI


Na Mwandishi Wetu, Mbinga, Ruvuma


Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imetenga jumla ya shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya maendelezo ya miundombinu ya barabara wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori wakati akielezea uendelezaji wa miundombinu ya barabara unaofanywa na TARURA wilayani humo.

Amesema ujenzi wa barabara kupitia Wakala huo umeweza kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao pamoja na kuinua uchumi katika halmashauri zote mbili za wilaya ya Mbinga.

“Wilaya ya Mbinga ni miongoni mwa kapu la chakula la Taifa kwani kuna uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara, mazao mengi ya chakula na biashara yanastawi kutokana na rutuba ya eneo hili”.

“Tunaishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anavyoendelea kutuletea fedha kupitia TARURA kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa miundombinu ya barabara na kuboresha mazingira”, ameongeza Mhe. Makori.

Aidha, amesema kwamba wilaya ya Mbinga kuna mabonde na milima kama kusingekuwa na uwekezaji wa Serikali kupitia TARURA hata uzalishaji wa mazao hayo ungekuwa tabu hususan kwenye kufikia maeneo ya uzalishaji. "Tunaishukuru Serikali inavyoleta fedha katika eneo la barabara”.
 
Hata hivyo, ameitaka TARURA kuendelea kuweka taa za barabarani katika maeneo mengine ili kupendezesha mji na kusaidia kuleta mazingira mazuri na kuongeza usalama kwa wananchi.

Pia, amewataka wananchi kuendelea kutunza barabara na miundombinu mingine ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Wananchi tushirikiane katika kutunza mazingira na barabara kwani ni uwekezaji mkubwa unafanyika katika maeneo yetu na kaleta ) maendeleo.
 
Kwa upande wa TACTIC Mhe. Makori amesema wilaya yake imepata miradi mitatu ikiwemo ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Km. 6 katika Mji wa Mbinga, ujenzi wa stendi mpya ya kisasa katika kata ya Lusaka pamoja na soko jipya na la kisasa.

“Kumekuwa na changamoto ya soko kwa muda mrefu kulingana na hadhi ya wilaya yetu hivyo kuja kwa mradi huu italeta mapinduzi makubwa katika upatikanaji na utoaji wa huduma kwa wananchi hivyo sisi tumekaa mkao mzuri wa kusubiri matunda mazuri yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita”.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakazi wa wilaya ya Mbinga wamefurahia uwekaji wa taa za barabarani kwani umewaongezea usalama na muda wa kufanya biashara.

Bw. Adrian Frank mkazi wa kata ya Masumuni amesema TARURA imewasaidia sana kwenye ujenzi wa miundombinu, kwani biashara zao sasa hivi wateja wanafurahia kwa kuwa kwa sasa hakuna vumbi ukilinganisha na zamani ambapo kulikuwa na matope na vumbi.

Ameongeza kuwa uwekaji wa taa umewasaidia kuondoa uhalifu kutoka Tanki la maji kwenda Mji Mwema kulikuwa na msitu hivyo kwa kuwekewa taa sasa hivi hawaogopi kutembea usiku na wanapita muda wowote hata usiku kurudi nyumbani. 

Naye, Bi. Christina Mapunda mkazi wa Mji Mwema ameishukuru Serikali kwa uwekaji wa taa kwani hivi sasa ile tabia ya uvunjaji wa maduka wakati wa usiku hakuna tena, pia hivi sasa wanatembea bila uwoga hata kama ni saa sita usiku mara wanapomaliza kufanya biashara zao.

No comments:

Post a Comment