Mkataba wa Euro milioni 34.86 sawa na takribani shilingi bilioni 96.47 kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa Kakono umesainiwa baina ya Serikali ya Tanzania pamoja na Shirika la Maendeleo la Ufaransa unaotarajiwa kukamilika mwaka 2026.
Mkataba huo umesainiwa leo Aprili 9,2024 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini Tanzania, Bi. Celine Robert.
Mradi huo utakaozalisha umeme wa megawati 87.8 kwenye gridi ya Taifa unaotarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali mnamo mwaka 2028 pia utaongeza uzalishaji wa umeme nafuu wa nguvu za maji ili kukabiliana na upungufu wa umeme katika gridi ya Taifa maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
‘’Mradi huu unafadhiliwa na Washirika watatu wa Maendeleo ambao ni AFD (Euro 110 milioni sawa na takriban TZS 304.37 bilioni), Benki ya Maendeleo ya Afrika (USD 161.47 milioni sawa na takriban TZS 413.95 bilioni) na Umoja wa Ulaya (Euro 34.86 milioni sawa na TZS 96.47 kusimamiwa na AFD) ambayo tumesaini leo’’, alisema Dkt. Mwamba.
Alisema kuwa Mradi wa Umeme wa Maji wa Kakono unaenda sambamba na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) wenye kaulimbiu ya kujenga Uchumi wa Kiushindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu kwa kuboresha miundombinu yenye tija, upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha biashara na uwekezaji, mazingira wezeshi pamoja na mifumo ya elimu na mafunzo.
Alisema kuwa mbali na mradi kusambaza umeme kwa watumiaji, pia unatarajiwa kutoa fursa za ajira takribani 1,000 zitatolewa wakati wa awamu ya utekelezaji pamoja na ajira 100 za kudumu wakati wa awamu ya uendeshaji na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa watu wanaozunguka mradi na kuboresha Maisha yao.
Dkt. Mwamba aliishukuru AFD kwa jitihada zote za kuhakikisha kwamba, ruzuku hiyo inapatikana kwa ajili ya mradi na kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na AFD na Washirika wengine wa Maendeleo ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa na kufikia lengo lililokusudiwa la maendeleo.
Mtambo unaotarajiwa kujengwa wa kufua umeme wa Kakono upo mto Kagera, takriban kilometa 90 magharibi mwa Manispaa ya Bukoba, ambayo ni kona ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania utakuwa mbadala wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ambayo hutumika kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini, Bi. Celine Robert, alisema kuwa mradi huo unaenda sambamba na malengo ya kimataifa ya tabia nchi na utasaidia Tanzania katika hatua ya kupunguza kiwango cha kaboni katika sekta ya nishati.
‘‘Mradi huu unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya eneo hili linalokua kwa kasi, ambalo liko katikati mwa eneo la Maziwa Makuu, kukuza uchumi wa viwanda na kuchochea ukuaji sio tu Tanzania bali hata katika nchi jirani,’’, alisema Bi. Celine Robert
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alisema Wizara hiyo kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) watahakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa.
Alisema mradi huo utarahisisha upatikaji wa umeme wa uhakika katika Mkoa wa Kagera na mikoa ya jirani, utaongeza ajira, utapunguza gharama za umeme na kuongeza mapato ya TANESCO.
Dkt. Mataragio alilipongeza Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali huku akiitaja baadhi ya miradi ya nishati iliyofadhiliwa na shirika hilo ikiwemo Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu, Mradi wa Umeme wa Jua Mafia pamoja na Mradi wa kuunganisha Tanzania na Zambia.
No comments:
Post a Comment