"Mnaposimamishwa na Askari wa Usalama Barabarani kupisha misafara ya viongozi tiini sheria na huo ndio uzalendo na utamaduni, msivunje sheria na kukaidi kwa kutumia udogo wa vyombo vyenu vya moto"
Kauli hiyo imetolewa Aprili 09, 2024 na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Boniphace Mbao wakati akizungumza na Maafisa Usafirishaji Umoja wa waendesha pikipiki na bajaji Dodoma (UMAPIDO) ambapo pamoja na hayo alisikiliza kero wanazo kutananazo madereva hao pindi wanapokua barabarani.
ACP Mbao amesema kuwa, Jeshi la Polisi lina thamini mchango wa Maafisa usafirishaji hivyo kwa yeyote ambae ana malalamiko na hajatendewa haki pindi anapo kumbwa na makosa ya usalama barabarani atoe taarifa kwa viongozi ili changamoto hizo ziweze kutatuliwa na kuzuiliwa zisijitokeze tena.
"Mnapoonywa na wasimamizi wa sheria za usalama barabarani zingatieni na mkarekebishe hayo makosa msikaidi kwani kufanya hivyo ni utovu wa nidhamu na kuendekeza makosa ya usalama barabarani kuendelea kuwepo."alisema ACP Mbao.
Vilevile, ACP Mbao amewataka maafisa usafirishaji hao kuhakisha wanakuwa na leseni za udereva na kuhudhuria mafunzo kabla ya kuingia barabarani na kutumia chombo cha moto kwani hayo ni matakwa ya sheria za usalama barabarani.
Pia, ACP Mbao amesema kuwa Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani limejikita zaidi katika utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wote wa barabara ili kuepuka ajali za barabarani zisizo tarajiwa.
Kwa upande wake Katibu wa umoja wa waendesha pikipiki na bajaji Remidius Flugence amewasihi Maafisa usafirishaji hao kuwa na leseni ya udereva pamoja na kujisajili katika vijiwe vya bodaboda.
Toka Dawati la Habari Dodoma.
No comments:
Post a Comment