USHIRIKIANO TANZANIA–MAREKANI KUIMARISHA UTAFITI NA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 21, 2026

USHIRIKIANO TANZANIA–MAREKANI KUIMARISHA UTAFITI NA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Tanzania itaendelea kunufaika na ushirikiano wa kimkakati na Serikali ya Marekani katika kuimarisha utafiti, uwekezaji na uendelezaji wa rasilimali madini, hususan madini ya kimkakati yanayohitajika kwa kiwango kikubwa duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 21, 2026 jijini Dodoma, mara baada ya kupokea ugeni kutoka Wizara ya Nishati na Madini ya Marekani, ulioongozwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, Waziri Mavunde amesema ushirikiano huo ni kielelezo cha mahusiano imara kati ya Tanzania na Marekani yaliyojikita katika ajenda za maendeleo ya pamoja.

Mavunde alisema kupitia ushirikiano huo, Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) itaendesha utafiti wa kina katika baadhi ya leseni zinazomilikiwa na STAMICO, kwa lengo la kubaini maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji wa madini.

“Zipo leseni zinazomilikiwa na STAMICO ambazo zitafanyiwa utafiti wa kina kwa kushirikiana na Wizara ya Madini ya Marekani ili kubaini maeneo yenye uwekezaji mkubwa. Hatua hii itaongeza uelewa, kuimarisha uhusiano wetu na kuinua uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania,” alisema Mavunde.

Aliongeza kuwa utafiti huo unatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara, maeneo yenye viashiria vikubwa vya uwepo wa madini ya kinye (graphite), ambayo mahitaji yake duniani yanaendelea kuongezeka kutokana na matumizi yake katika teknolojia za kisasa, ikiwemo nishati mbadala na magari ya umeme.

“Makadirio yanaonesha kuwa ifikapo mwaka 2050, mahitaji ya graphite yatafikia tani milioni 4.5 kwa mwaka. Tanzania iko katika nafasi nzuri kuwa miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa madini haya duniani,” alisema.

Waziri Mavunde alibainisha kuwa pamoja na utafiti wa madini, ushirikiano huo utawezesha kujengewa uwezo wataalamu wa Kitanzania kupitia mafunzo ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika utafiti wa madini na uchambuzi wa taarifa za kijiolojia, hatua itakayoongeza uwezo wa nchi kusimamia rasilimali zake kikamilifu.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, alisema Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya madini, ili kuhakikisha utafiti wa kina unafanyika na fursa za uwekezaji zinabainishwa kwa manufaa ya pande zote.

“Kwa kushirikiana na STAMICO, tutafanya utafiti wa kiwango cha upatikanaji wa madini ya kinywe katika mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na kuwajengea uwezo Watanzania kuhusu mchakato mzima wa utafiti,” alisema Lentz.

Alisisitiza kuwa ushirikiano huo una lengo la kusaidia Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali zake, kuvutia uwekezaji mkubwa na kuchangia katika ukuaji wa uchumi endelevu.

Hatua hiyo inaendelea kudhihirisha dhamira ya Tanzania na Marekani kuimarisha ushirikiano wa maendeleo katika sekta ya madini, sambamba na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment