SERIKALI YATAKA CBE KUZALISHA WATAALAMU BUNIFU KUSAIDIA SEKTA YA UTALII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 21, 2026

SERIKALI YATAKA CBE KUZALISHA WATAALAMU BUNIFU KUSAIDIA SEKTA YA UTALII



Serikali imekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuelekeza nguvu katika kuzalisha wataalamu wabunifu na wenye ujuzi wa hali ya juu watakaoweza kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya utalii, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dennis Londo (Mb.) akiwa ameambatana na Viongozi mbalimbali wakati wa ziara yake ya kukagua eneo linalotarajiwa kujengwa Kampasi ya CBE Kilimanjaro lililopo wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.

Amesema kampasi hiyo inatarajiwa kuwa sehemu ya majibu ya changamoto za kimuundo na kitaalamu zinazokabili sekta ya utalii, kwa kuandaa wataalamu watakaobobea katika biashara ya utalii na shughuli zote zinazohusiana, ikiwemo ukarimu, ujasiriamali, masoko ya utalii na usimamizi wa biashara za utalii.

“Tunatambua umuhimu mkubwa wa sekta ya utalii katika mapato ya Taifa na ajira, ndio maana tunataka CBE izalishe wataalamu watakaosaidia kuongeza thamani ya sekta hii, siyo kama waajiriwa pekee bali pia kama wamiliki na wabunifu wa makampuni na miradi ya utalii,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Tandi Lwoga, amesema kampasi ya Kilimanjaro itakuwa kampasi ya tano ya chuo hicho nchini na itachangia kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekta ya biashara.

Amesema kuwa kwa sasa wana Wanafunzi 24,657 na chuo hicho kikikamilima itaongeza zaidi ya Wanafunzi 2000.

Amesema usanifu wa majengo matatu ya awali tayari umeanza ikijumuisha madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,000, hoteli ya nyota tatu yenye uwezo wa kulaza wageni 52 kwa wakati mmoja pamoja na mabweni ya wanafunzi.

Amesema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu (Higher Education Transformation Project) una thamani ya Sh bilioni 17.4, na baada ya taratibu za kifedha kukamilika, ujenzi wa kampasi unatarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment