Shirika la ndege la Kenya Airways limepinga kukamatwa na kuzuiliwa kwa wafanyikazi wawili huko Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wawili hao, kulingana na KQ walikamatwa kwa madai ya kupotea kwa hati za forodha za shehena iliyokuwa isafirishwe na shirika hilo la ndege.
Shirika la ndege la Kenya Airways, hata hivyo, lilisema shehena husika haikuinuliwa au kukubaliwa nao kutokana na kutokamilika kwa nyaraka.
Shirika hilo la ndege lilisema wakati wa kukamatwa, simu zao zilichukuliwa na walikataliwa kuwasiliana na mtu yeyote.
Walikamatwa na Kitengo cha Ujasusi cha Kijeshi.
"Kenya Airways (KQ) inathibitisha kwamba mnamo Ijumaa, Aprili 19, 2024, wafanyikazi wetu wawili katika afisi yetu ya uwanja wa ndege huko Kinshasa walikamatwa na wanaendelea kuzuiliwa na Kitengo cha Ujasusi cha Kijeshi kinachojulikana kama Detection Militaire des Activities Anti Patrie (DEMIAP), " KQ ilisema katika taarifa siku ya Ijumaa.
Shirika hilo la ndege lilisema wakati maafisa wa Ubalozi wa Kenya na wafanyakazi wachache waliruhusiwa kuwatembelea ni kwa dakika chache tu.
Ilisema kuwa wakati mahakama ya Kijeshi ilisikiliza kesi hiyo na kuamuru waachiliwe bila masharti, siku ya Alhamisi, bado wako kizuizini.
"Licha ya maagizo ya mahakama, kitengo cha kijasusi cha kijeshi bado kinawashikilia kwa siri, lakini hawa ni raia wanaozuiliwa katika kituo cha kijasusi cha kijeshi." shirika la ndege lilisema.
Mkurugenzi Mtendaji Allan Kilavuka katika taarifa hiyo alisema shehena hiyo bado ipo kwenye sehemu ya mizigo ikifanyiwa kibali ndipo kikosi cha ulinzi kilifika na kuwachukua wafanyakazi hao wawili kwa mahojiano.
Alibainisha kuwa walidai kuwa shirika hilo la ndege lilikuwa likisafirisha mizigo bila kibali cha forodha na jitihada za kueleza kuwa hawakukubali mizigo hiyo ziliambulia patupu.
"Mzigo huo haukuwa angani kwa usafiri na, kwa hivyo, haikuwa mikononi mwa KQ kwani mhudumu wa vifaa alikuwa bado anakamilisha stakabadhi kabla ya kuikabidhi kwa KQ," Kilavuka alisema.
Kenya Airways ilisisitiza kuwa inazingatia kanuni bora za kimataifa katika kushughulikia na kusafirisha mizigo, wakati wote.
Shirika hilo la ndege liliongeza kuwa lina taratibu kali na ukaguzi wa kufuata unaojulikana kama 'Tayari kwa ajili ya kubeba' ili kuhakikisha shehena yoyote inayobebwa kwenye safari zao za ndege inakidhi mahitaji yote ya kisheria kote tunakoenda.
"Washirika wetu wote wa ugavi lazima watii hatua hizi kabla ya KQ kukubali shehena yoyote."
No comments:
Post a Comment