WAZIRI MKUU: MAHAKAMA ZAANZA KUTUMIA MFUMO WA KUTAFSIRI LUGHA ZA KIINGEREZA NA KISWAHILI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 16, 2024

WAZIRI MKUU: MAHAKAMA ZAANZA KUTUMIA MFUMO WA KUTAFSIRI LUGHA ZA KIINGEREZA NA KISWAHILI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mahakama zimeanza kutumia mfumo unaonasa sauti na kuzibadilisha kwenda kwenye maandishi huku ukitafsiri lugha za Kiingereza na Kiswahili. 

“Hii ni hatua kubwa sana kwani mfumo huo unarekodi sauti na kupeleka kwenye maandishi. Vilevile, unaweza kutafsiri lugha ya Kiswahili au Kiingereza kulingana na uhitaji,” amesema na kuongeza: “Kanuni za Mahakama zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihutasari ya hukumu kwa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri.”

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumatatu, Aprili 15, 2024) Bungeni, jijini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2024/2025.

Akielezea mambo yaliyofanyika ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu amesema mbali ya matumizi ya Kiswahili mahakamani, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kutokana na mapinduzi ya nne ya viwanda duniani. 


“Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake) ziweze kusomana kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio mfano: Mahakama ya Tanzania, ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.”  

Waziri Mkuu ameitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Usajili, Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa mashauri mahakamani. 

“Mfumo mwingine ni wa unukuzi na kutafsiri mienendo ya mashauri Mahakamani kwa lengo la kuwa suluhu ya kudumu ili kuwawezesha Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuondokana na adha ya kuandika kwa mkono mwenendo wa mashauri,” ameongeza. 


Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha mfumo wa utoaji haki unaboreshwa, Januari 31, 2023, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda Tume maalum aliyoipa jukumu la kushauri namna njema ya kuboresha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.

Akielezea maboresho ya mfumo wa utoaji haki na taasisi za hakijinai, Waziri Mkuu amesema: “Tume hiyo, ilipokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine wa hakijinai na kutoa mapendekezo ya maboresho yanayohitajika kufanyika. Tangu Tume ilipowasilisha mapendekezo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za maboresho ya mfumo wa utoaji wa hakijinai ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa taasisi za hakijinai.” 

Amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao kwa wakati na waweze kuendelea kufanya shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa zima kwa ujumla. 

“Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukidhi kiu na matarajio ya wananchi ya utoaji wa hakijinai kuanzia hatua za uchunguzi, ukamataji wa watuhumiwa hadi utoaji wa hukumu yenye haki mahakamani,” amesisitiza.
  
Kwa mwaka 2024/2025, Bunge limeidhinisha sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.

Vilevile, Bunge limeidhinisha sh. 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.


No comments:

Post a Comment