Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua Nembo ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, hafla iliyofanyika leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma. |
Na Okuly Julius - Dodoma
Ametoa maelekezo hayo Leo Aprili 8,2024 Jijini Dodoma wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Nembo na kauli mbiu ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia amewataka watanzania kuendelea kuulinda Muungano kwani ni kichocheo cha Maendeleo
“Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla ,Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla.“amesema Mhe.Majaliwa
Aidha, amesema katika maadhimisho ya mika 60 ya muungano mwaka huu yatahushishwa shughuli mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa miradi mbalimbali utakaofanywa na viongozi wakuu wa serikali wa pande zote za muungano.
Majaliwa amesema kuwa Aprili 14 mwaka huu Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyeki baraza la Wawakilishi Dk.Husein Alli Mwinyi anatarajiwa kuzindua rasmi maadhimishi hayo.
“Mara baada ya tukio hilo miradi mbalimbali itazinduliwa na viongozi wa mbalimbali wa kitaifa katika pande zote za muungano”amesema Majaliwa
Ametaja tukio jingine ni maombi ya kitaifa kuombea muungano ambayo yatafanyika Aprili 22 kitaifa jiji Dodoma yakiongozwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
“Niagize wakuu wa mikoa yote kuhakikisah kuwa wanaratibu maombi haya ili kila mkoa ushiriki katika maombi haya ya kuuombea mungano wetu”
Pia amezitaka taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano wetu kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza.
Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia kilele cha sherehe za Muungano katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam
“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.“amesema
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Jenisita Mhagama amesema miaka 60 ya muungano Tanzania inajivunia kwa kuwa na Rais wa kwanza mwanamke.
"Muungano huu ni sawa na Jubelei ya Almasi, hivyo, haina budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha kwa furaha miaka hiyo 60," amesema Mhagama
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ,Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma amesema kuwa Muungano ndio tunu kubwa iliyobakia hivyo ni vyema kila mmoja kuulinda,kuuenzi na kuutunza kwa gharama yeyote Ile.
Pia amewataka Watanzania kuwaenzi Waasisi wa Muungano Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambaye Aprili 07, 2024 ilikuwa kumbukizi ya miaka 52 ya kifo chake.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Watanzania wana kila sababu ya kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amewataka Watanzania kutembea kifua mbele kujivunia Muungano huo adhimu ambao umeleta faida lukuki zikiwemo uhusiano mzuri baina ya wananchi wa pande zote mbili katika Nyanja mbalimbali.
Waziri Dkt. Jafo amewashukuru na kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa usimamizi wao na kuwezesha utatuzi wa changamoto 15 kati ya 18 ndani ya miaka mitatu ya uongozi wao.
No comments:
Post a Comment