Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi Duniani kote wameungana kwa pamoja kusheherekea Siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo leo Mei 01,2024 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewafurahisha watumishi wa Umma kwa kuonesha nia ya Serikali ya kuendelea kuwapandisha madaraja, kuendelea kuongeza mishahara na kuboresha mazingira ya watumishi.
Dkt. Mpango ameyasema hayo Jijini Arusha katika Sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika Kitaifa Jijini humo ambapo ameonesha nia ya Serikali ya kuboresha maisha ya watumishi wa Umma na watumishi wa Sekta Binafsi ikiwemo kupandisha madaraja na kuboresha mishahara kwa watumishi wa Umma na watumishi wa Sekta Binafsi hususan kwa watumishi wa kada ya chini.
Kwa upande wa Makao Makuu ya Nchi Jijini Dodoma, Sherehe hizo zimefanyika katika kiwanja cha Jamhuri Jijini humo ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameshiriki kama Mgeni Rasmi wa sherehe hizo.
Pamoja na mambo mengine, Senyamule ametoa salamu za Rais katika sherehe hizo ambapo amesema Rais Samia anawapenda watumishi wote wa Taasisi za Umma na Taasisi binafsi na kuwataka kuwa watulivu wakati Serikali ikifanyia kazi maboresho ya watumishi wote wa Umma na Sekta Binafsi.
Katika hatua nyingine, Senyamule amewataka Watumishi wote nchini kuchapa kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuleta ufanisi katika kazi zao kwa lengo la kuleta maendeleo chanya ya Taifa.
Aidha, ndugu Muadhi Mayunga ambaye ni afisa utumishi katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ameibuka kuwa mfanyakazi Hodari katika Taasisi hiyo kwa kutimiza majukumu yake kwa weledi na ufanisi kwa mujibu wa mpangilio wa majukumu yake.
Sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Kitaifa imebebwa na Kaulimbiu isemayo Nyongeza ya Mshahara ni Msingi wa Mfano Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha ambapo Kidunia imebebwa na Kaulimbiu isemayo Ensuring Safety and Health at Work in a Changing Climate 2024.
No comments:
Post a Comment