Ndani ya darasa lenye shughuli nyingi la shule ya msingi katika mji wa pwani wa Afrika Kusini wa Saldanha Bay, kiti kimoja kiko kitupu.
Hapa ndipo Joshlin Smith mwenye umri wa miaka sita aliketi hadi alipotoweka mwezi Februari katika kesi ambayo imeteka hisia za Waafrika Kusini.
Operesheni kubwa ya utafutaji iliyohusisha jeshi la wanamaji pamoja na wafanyakazi wa kujitolea wa ndani, zawadi kubwa na kukamatwa kwa mama yake kumesaidia kufanya hii kuwa hadithi isiyozuilika.
Lakini jamii inayoishi na ukweli wake wa kila siku inabaki na hofu.
Saldanha Bay, takribani kilomita 120 (maili 75) kaskazini-magharibi mwa Cape Town, ina sifa ya kuwa mji tulivu, wa ajabu unaojulikana kwa uvuvi, michezo ya maji na maua ya porini yenye rangi nzuri ambayo huchanua majira ya kuchipua katika hifadhi ya asili ya mji huo.
Licha ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi miaka 30 iliyopita, mipango katika Saldanha, kama miji mingi nchini Afrika Kusini, bado inaonesha ukosefu wa usawa ulioachwa na mfumo wa maendeleo tofauti na yasiyo sawa.
Mtu anapoingia mjini kupitia eneo la biashara, nyumba ya juu, ambayo inajumuisha nyumba za wageni na nyumba za likizo, iko karibu na ukanda wa pwani.
Lakini wakati wa kwenda katika maeneo ya Diazville na Middelpos, ambayo yanajumuisha mchanganyiko wa nyumba za gharama nafuu na zisizo rasmi, kuna mabadiliko yanayoonekana.
Nyumba katika Diazville nyingi ni miundo ya msingi ya matofali na chokaa inayofadhiliwa na serikali, inayojulikana kama nyumba za RDP (sehemu ya Mpango wa Ujenzi na Maendeleo). Katika eneo la karibu la Middelpos kuna mchanganyiko wa nyumba za RDP na vibanda vya bati vilivyojengwa kwenye uwanja wazi.
Kuna hali ya wasiwasi na mashaka katika jumuiya hizo mbili, hasa wanapoona mtu wa nje au gari ambalo halitoki eneo hilo.
Ongezeko la idadi ya wazazi na walezi wanaosubiri kwa hamu kuwachukua watoto wao nje ya lango la shule ya msingi ya Diazville ni dalili ya jinsi wakazi wanavyochukuliwa tahadhari zaidi ili kuhakikisha usalama wa watoto wadogo katika eneo hilo.
Kuwafanya watu wazima hao wazungumze si rahisi.
Kusitasita huko kunaeleweka kutokana na mihemko kwa vyombo vya habari, na visa kadhaa vya habari za uwongo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kama vile madai ya kuonekana na ripoti za kupatikana kwa mwili.
Faeeza Ecksteen, mmoja wa wazazi waliokuwa tayari kuzungumza, alikuwa katika shule aliyosoma Joshlin kumchukua mtoto wake wa kiume wa miaka sita Aleem. |
Anasema kutoweka kwa Joshlin kumekuwa na athari kubwa kwa jamii, haswa watoto.
"Ni hadithi ya kusikitisha sana. Wazazi wote sasa wana wasiwasi kuhusu ustawi wa watoto wao na wanachukua tahadhari zaidi ili kuhakikisha usalama wao."
"Inahuzunisha watoto katika eneo hilo kwa sababu hawataki tena kucheza nje," anaongeza mwanaharakati wa jamii Carmelite Ross.
"Binti yangu mwenye umri wa miaka 11, Keayondre, hakutaka kwenda shule kwa siku chache za kwanza baada ya kutoweka kwa Joshlin kwa sababu alikuwa na hofu, ingawa shule iko umbali wa dakika chache. Sasa anatembea kwenda shuleni kila siku na watoto wengine sita.
"Mwisho wa siku kila mtu huko Saldanha, hata watoto wetu, wameguswa na suala hili."
Bi Ross, ambaye alishiriki katika utafutaji wa Joshlin katika siku chache za kwanza baada ya kutoweka kwa binti mdogo, aliamua kurudi nyuma kwa ajili ya ustawi wake.
"Niliamua kupunguza ushiriki wangu katika kesi ya Joshlin kwa sababu ilianza kunisumbua sana.
"Kama mama mwenyewe, inatia uchungu sana.
Nimekuwa nikikosa usingizi kwa sababu angekuwa mtoto wangu sidhani kama ningekuwa hai kutokana na wasiwasi, msongo wa mawazo na kila kitu ambacho unapaswa kukabiliana nacho."
Wiki mbili baada ya Joshlin kutoweka kwenye kibanda chake cha kawaida katika makazi yasiyo rasmi ya Middelpos, polisi walimkamata mama yake Racquel "Kelly" Smith, mpenzi wa Smith Jacquen "Boeta" Appollis, Steveno van Rhyn na Phumza Sigaqa.
Nyumba hiyo tangu wakati huo imefungwa.
Wanne hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya eneo hilo tarehe 7 Machi kwa mashtaka ya ulanguzi wa binadamu na utekaji nyara. Umati mkubwa wa watu wa eneo hilo walikusanyika karibu na mahakama kutoa wito wa "haki kwa Joshlin".
Siku chache za kwanza baada ya kutoweka kwake kuliandamana na mvutano wa rangi kati ya watu wa rangi (kama watu wa kabila mchanganyiko wanavyojulikana nchini Afrika Kusini) na watu weusi wa jumuiya hiyo kufuatia kukamatwa kwa Bi Sigaqa, mtu mweusi.
Alinaswa katika uvumi na ripoti za vyombo vya habari zilimtambulisha kimakosa kama mganga wa kienyeji, au sangoma.
"Kuna siku ambapo watu wa eneo hili walitutaja kama sisi ndio sababu za kutoweka kwa Joshlin. Kuna siku ambapo watu walikuwa na mashaka na sangoma, wakifanya mambo mabaya," Liwani Siyabulela, diwani wa wadi ya Middelpos, anaiambia BBC.
"Tumeweza kushughulikia masuala, tumeweka wazi kuwa sio rangi au nyeusi au nyeupe, Mhindi au chochote. Tunapaswa kuzingatia kutafuta mtoto aliyepotea. Angalau sasa hali imerejea kawaida," Anasema Bi Siyabulela, mwanachama wa chama tawala cha African National Congress (ANC).
Bi Ross anakiri huenda kulikuwa na mivutano ya rangi hapo awali lakini anafurahi kwamba ilitatuliwa haraka.
"Sijawahi kupata umoja wa namna hii katika jumuiya hii. Kila mtu, bila kujali kabila au tamaduni gani, wote walikuwa pale wakisaidia katika utafutaji. Niliona umoja katika watu wetu."
Bi Sigaqa ameachiliwa baada ya mashtaka dhidi yake kuondolewa kutokana na ukosefu wa ushahidi. Tangu wakati huo ameondoka nyumbani kwake ambako ni mita chache tu kutoka alipokuwa akiishi Joshlin kufuatia vitisho kutoka kwa wanajamii.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32 alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha taifa cha Newzroom Afrika kwamba polisi walimtesa alipokuwa kizuizini. Polisi hawajajibu tuhuma hizo.
Lourentia Lombaard, ambaye aliripotiwa kuwa mtu wa mwisho kumuona Joshlin kabla ya kutoweka, alikamatwa baadaye na bado yuko kizuizini.
Kulingana na msemaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Mashtaka Eric Ntabazalila, Bi Lombaard amekiri kosa ingawa habari zaidi zitatolewa baadaye.
Wengine watatu waliokuwa kizuizini hawajazungumzia mashtaka hayo, lakini Bi Smith awali alikuwa ameliambia gazeti la ndani la The Daily Voice kwamba hakuwa amekata tamaa ya kumpata binti yake.
“Msukumo wangu wa kimama unaniambia binti yangu bado yuko hai na eneo hili tutampata, nitatembea kwa miguu kumtafuta. Nitaangalia kwenye kila kibanda kidogo, nitafanya peke yangu."
Kutoweka kwa watoto kunaendelea kusumbua jamii ya Afrika Kusini.
Kulingana na Bianca van Aswegen, mratibu wa kitaifa wa Shirika la Watoto Waliopotea Afrika Kusini (MCSA), takwimu zilizotolewa na ofisi ya watu waliopotea nchini humo mwaka 2013 zilisema kuwa mtoto hupotea kila baada ya saa tano nchini, lakini hazijasasishwa tangu wakati huo.
Takwimu za MCSA zinaonesha kuwa zaidi ya robo tatu ya watoto hao wanapatikana lakini wengine wanashukiwa kusafirishwa au kuuawa.
"Inaweza kuwa kesi ya Joshlin ilikumba mitandao ya kijamii kwa dhoruba. Kwa bahati mbaya, watu wengi walieneza habari za uwongo katika mchakato huo ambao umetatiza uchunguzi," asema Bi Van Aswegen.
Kurudi katika shule ya Joshlin kila mtu ana matumaini kwamba atapatikana akiwa hai.
Kwenye ukuta wa ukumbi wa kuingilia kuna mkusanyiko wa ujumbe wa usaidizi kutoka kwa madarasa tofauti kando ya picha yake.
Shule hiyo pia imechapisha video kwenye ukurasa wake wa Facebook ambapo mkusanyiko wa watoto huimba "Mungu atalifanyia kazi".
Lakini wanafunzi wachanga pia wanahitaji kutafuta njia ya kujilenga wenyewe, mkuu wa shule Lee-Ann Davids-Hartzenberg anasema.
"Bado tunatumai na kumuombea Joshlin arejee salama, lakini tunahitaji kufanya kazi na kufanya kazi kila siku kwa uwezo wetu wote. Tunahitaji kusonga mbele. Mambo ni mazuri muhula huu lakini wanafunzi wenzake Joshlin bado wanamkosa darasani.
"Wanaimba mara kwa mara wimbo ambao aliupenda na pia wanapanda mmea kwa ajili yake darasani."
No comments:
Post a Comment