Waasi wa M23 wanasema wameuteka mji wa uchimbaji madini katika eneo la Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini, baada ya mapigano makali na jeshi Jumanne na Jumatano asubuhi.
Rubaya ni mojawapo ya maeneo muhimu ya uchimbaji madini ya coltan duniani, madini haya adimu ni muhimu katika uzalishaji wa simu za mkononi, kompyuta, na magari ya umeme.
"Tumechukua eneo hilo [Rubaya] si kwa sababu ya utajiri wake, lakini kumfukuza adui yetu ambaye analenga kufanya mauaji ya kimbari. Lengo letu si migodi bali kuokoa maisha ya watu”, Willy Ngoma msemaji wa jeshi la waasi aliambia BBC.
Hata hivyo, jeshi la Kongo halikuzungumzia madai ya waasi hao.
Rais wa jumuiya ya kiraia ya Masisi, Voltaire Sadiki, aliiambia BBC kwamba waasi wameteka mji wa Rubaya, na "kuamuru raia wenye bunduki kuwakabidhi na kuendelea na maisha yao", alisema.
Siku ya Jumanne wakati mapigano yalipokuwa yakiendelea huko Rubaya, Rais Felix Tshisekedi wa DR Congo alikuwa Paris ambako alikariri kwa nguvu kwamba jeshi la Rwanda liko nyuma ya M23, na Rais wa Ufaransa Macron aliitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake kutoka DR Congo.
Rwanda inakanusha kuunga mkono M23 na Rais Paul Kagame amemshtumu Bw Tshisekedi kwa kushindwa kushughulikia masuala ya wakimbizi wa Kongo katika eneo hilo na M23 kama matatizo ya Kongo.
Rubaya, mwendo wa saa mbili kwa gari kuelekea magharibi kutoka Goma, iko katikati ya uchimbaji haramu wa madini ya coltan, madai ya ajira ya watoto, na biashara haramu ya makundi mbalimbali yenye silaha.
Licha ya kuwa na maliasili nyingi, wakazi wa Rubaya, na DR Congo kwa ujumla, wanaishi katika umaskini, ripoti za wataalamu mbalimbali zinasema.
No comments:
Post a Comment