Na Mwandishi Wetu, Beijing
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) aliyeko ziarani nchini China ameyashawishi makampuni makubwa ya utalii nchini hapa kuwekeza katika shughuli za utalii nchini Tanzania ikiwemo kuleta watalii.
Ameyasema hayo jijini Beijing katika mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Masuala ya Sheria na Utalii ya Yingke (Yingke Group), Mei Xiang Rong ambaye kampuni yake inatoa ushauri katika maeneo hayo kwa kampuni zaidi ya 2,000 duniani ikiwemo kupeleka watalii sehemu mbalimbali na kuwekeza katika mahoteli.
Wito kama huo ameutoa pia leo Mei 14, 2024, katika kikao kingine na kampuni ya kitalii ya YCMS Travel inayosafirisha takribani watalii Milioni 20 kwa mwaka kutoka China kwenda nchi mbalimbali ambao wameahidi pia kuleta watalii Tanzania na pia kuitangaza filamu mpya ya “Amazing Tanzania.”
Vikao hivyo pia vimehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma na binafsi.
Waziri Kairuki yuko nchini China kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na China pamoja na uzinduzi wa mwaka wa Utalii na Utamaduni na pia uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” utakaofanyika Mei 15, 2024 jijini Beijing.
No comments:
Post a Comment