Mwanamke wa Australia aliyedaiwa kuwaua watu watatu kwa kuwalisha uyoga wenye sumu kwenye chakula cha mchana amekanusha shitaka la mauaji.
Erin Patterson, 49, anakabiliwa na mashtaka matatu ya mauaji na makosa mawili ya kujaribu kuua mnamo Julai mwaka jana.
Polisi pia wanadai kuwa alijaribu kumuua mumewe aliyeachana naye katika matukio mengine matatu.
Bi Patterson daima amedumisha kutokuwa na hatia.
Amekuwa akisema mara kwa mara hakuwatilia sumu wageni wake kwa makusudi, na Jumanne katika Mahakama ya Latrobe Valley aliombwa kujibu rasmi mashtaka dhidi yake.
"Sina hatia mheshimiwa," alisema, akionekana kupitia video.
Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa katika maeneo mengi ulimwenguni.
Bi Patterson aliandaa chakula cha mchana nyumbani kwake huko Leongatha - kusini-mashariki mwa Melbourne - tarehe 29 Julai.
Waliohudhuria walikuwa wakwe zake wa zamani Gail na Don Patterson, pamoja na dada ya Gail Heather Wilkinson na mume wa Heather Ian.
Polisi wamesema mume wa Bi Patterson aliyeachana naye Simon Patterson pia alialikwa lakini hakuweza kufika dakika za mwisho.
Saa kadhaa baada ya kula chakula hicho, wageni wote wanne waliugua kwa kile walichofikiri ni sumu kali ya chakula.
Baada ya siku chache, wanandoa wa Patterson, wote 70, na Bi Wilkinson, 66, walifariki dunia. Bw Wilkinson, 68, alinusurika, baada ya kukaa karibu miezi mitatu hospitalini.
Polisi wanasema wanaamini kuwa wanne hao walikula aina ya uyoga - ambao ni hatari sana unapomezwa.
Bi Patterson alitajwa na polisi kuwa mshukiwa kwa kuonekana kuwa yeye hakudhurika popote baada ya chakula hicho cha mchana.
Baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa, wapelelezi walidaiwa kufichua majaribio mengine matatu ya mauaji ambayo Bi Patterson aliyafanya dhidi ya mumewe waliyeachana kati ya 2021 na 2022, na mnamo Novemba alikamatwa na kushtakiwa rasmi kwa makosa manane kwa jumla.
Kesi yake sasa itafuatiliwa kwa haraka katika Mahakama ya Juu Zaidi ya Victoria huko Melbourne huku kusikilizwa kwake kwa mara ya kwanza kukipangwa kuwa tarehe 23 Mei.
No comments:
Post a Comment