Kocha mkuu wa Kikosi cha Yanga SC Miguel Gamondi ameongea kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi kuu ya NBC dhidi ya Tabora United.
Amesema kuwa, ana matumaini makubwa ya kuwapa burudani mashabiki wake na kuwataka waje wafurahie.
"Nafahamu mashabiki wetu kesho wanatamani kupata burudani ya kutosha, nina matumaini makubwa sana kuwa watapata burudani, sitawaangusha kwani kila mara wamekuwa wakitoa mchango wao mkubwa kwetu. Njooni kwa Mkapa Wananchi mtafurahi,”
"Mimi nawaamini wachezaji wangu ndio maana nafanya mabadiliko ya mara kwa mara. Najaribu kuwapa nafasi wengine kufanya kile walicho nacho kwa sababu wote wananipa kila ninachokitaka kwenye Uwanja wa mazoezi," amesema Gamondi.
Nae mchezaji na beki wa kikosi cha Yanga SC Ibrahimu Bacca amezungumza kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Tabora United huku akisema kuwa atashangaa kama kuna shabiki wa Yanga SC hatafika uwanjani siku ya kesho.
"Nitashangaa kama kuna shabiki wa Young Africans hatafika Uwanjani hapo kesho. Matukio kama haya ni matukio ambayo yanayokea mara chache na mashabiki wanajua wapi tulipotoka na kama wachezaji tupo tayari kazi imebaki kwenu Wananchi kujitokeza kwa wingi,”
"Haijalishi ni nani atapewa nafasi ya kucheza, sisi wenyewe tunaaminiana, tunafahamu kila mchezaji anayecheza Young Africans ana mchango mkubwa kwa Klabu yetu. Kwa maana hiyo kila mchezaji atakayepata nafasi basi ataonyesha ubora aliokuwa nao,” amesema Bacca.
Aidha amesema wachezaji wamejiandaa vizuri kwa kufanya mazoezi ya kutosha ili waweze kutoa burudani kwa mashabiki kabla ya burudani ya baada ya mpira hivyo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi.
Ikumbukwe kuwa mchezo wa kesho ndiyo mchezo ambao Yanga SC atakabidhiwa kombe kusheherekea ubingwa wa 30 wa klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment