SULUHISHO VIKUNDI VYA KIJAMII KUTUNZA FEDHA YAPATIKANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 3, 2024

SULUHISHO VIKUNDI VYA KIJAMII KUTUNZA FEDHA YAPATIKANA



Na WMJJWM, Dar Es Salaam

Vikundi mbalimbali vya kijamii vimehimizwa kuweka fedha katika akaunti za benki kwa usalama ili kutimiza malengo yao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua Akaunti ya Kikundi ya Benki ya NMB ili kuwezesha vikundi mbalimbali vya kijamii kujiendesha, katika hafla iliyofanyika jijini Dar Es Salaam Mei 3 2024.

Amesema Benki ya NMB imekuja na suluhisho mbadala katika utoaji huduma za kibenki hususani kwa vikundi vya kijamii vya kuweka akiba na kukopa na kuhimiza wanavikundi kufuatilia akaunti hiyo.


"Nina imani hatua hii ya kuanzishwa kwa huduma ya akaunti kwa vikundi inakwenda kuziba pengo lililopo kati ya taasisi za fedha na makundi yasiyo rasmi ya akiba kwa kusogeza huduma za fedha karibu yao na kwa usalama mkubwa zaidi wa fedha zao na hii itaongeza chachu kwa wananchi wengi walio katika vikundi na hususan vya wanawake kutumia huduma za kibenki." amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Aidha ameeleza mikakati ya makusudi inayofanywa na Serikali kuhakikisha idadi ya watu wanaotumia huduma za kifedha kama benki inaongezeka ikiwemo mpango wa Taifa wa Huduma jumuishi za Kifedha na  
usimamizi mzuri wa utoaji wa huduma za fedha hususan katika benki. 


Ameongeza kwamba, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo kiwango cha watu walio nje ya huduma rasmi za kifedha bado kipo juu kwa baadhi ya makundi yakiwemo ya wanawake, wakulima wadogo na vijana ambao wengi wao ni wakazi wa maeneo ya vijijini, hivyo Serikali imeendelea kuwekeza katika matumizi ya Teknolojia ili kuleta uwiano sawa katika upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha nchi nzima na kuhakikisha makundi yote yananufaika na huduma za fedha.

Waziri Dkt..Gwajima pia ametoa wito kwa benki ya NMB kuyatumia Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwani ni ya muhimu yakitumika kikamilifu katika kuwafikia wananchi hasa wanawake na yatakuwa kiungo kati ya benki na vikundi kwa kuwa majukwaa yanaundwa kutokana na vikundi.  

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema lengo la kufungua akaunti hiyo ni kuboresha akaunti iliyozinduliwa mwaka 2020 kwa jina la Pamoja akaunti kuwa ya kidijitali zaidi.

Amesema akaunti hiyo sasa ina manufaa zaidi na kuwezesha vikundi kuongezeka kufikia laki 2 vyenye wanachama zaidi ya miilioni moja ambapo amebainisha kuwa ni jukumu lao kuhakikisha wanaleta suluhisho kwa wateja la usalama wa fedha zao.

Nao baadhi ya wanufaika wa akaunti ya NMB Kikundi akiwemo mtangazaji maarufu Dina Marius wamebainisha umuhimu wa kuhifadhi fedha benki hasa katika vikundi vya kijamii kwani kuna wasaidia kuwa na uhakika wa fedha zao badala ya kuzihifadhi majumbani.

No comments:

Post a Comment