Na Carlos Claudio, Dodoma.
Taasisi ya Shule Direct imetoa mafunzo na kuhamasisha jamii kuhusiana na elimu jumuishi kwa kushirikisha wanajamii katika kufanya uhamasishaji.
Wabeba bendera hao wa pamoja katika Elimu jumuishi wameishukukuru Taasisi hiyo kwa elimu pamoja na kuibua watu wenye mahitaji maalumu pamoja na kufanya uchechemuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dodoma
katika hafla ya ufungaji wa mradi wa Taasisi ya Shule Direct ambayo inatekeleza mradi wa pamoja katika elimu jumuishi wameeleza kuwa wataendelea kuelimisha jamii bila kukoma.
Diwani viti Maalum kutoka Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Sada Omary anaeleza kuwa mradi huo umeleta hamasa kwa jamii kwa sababu umeweza kuona vikundi mbalimbali ambavyo vimewatembelea na kutoa elimu.
Amesema jamii imeweza kuelimika na kutambua haki za watu wenye mahitaji maalumu pamoja na kuzingatia wahitaji hao wanapata haki zao katika jamii inayowazunguka.
"Sisi tunaozunguka huko Vijijini tutajitahidi kueneza elimu mliyotuachia kwa sababu hamkafanya kazi bure bali mmefanya kazi yenye matunda,” amesema Sada.
Naye Afisa Maendeleo kata ya Miyuji Halmashauri ya jiji la Dodoma Yunis Mweta amewashukuru wote ambao wamejitolea na kuwaibua watu wenye mahitaji maalum kwani kata ya Miyuji imefanikiwa kuibua na wameweza kuunganishwa na huduma huku ikiendelea kupata huduma hizo.
“Kupitia mradi huu jamii imeweza kufumbuka pamoja na kuwazingatia watu wenye mahitaji maalumu kwa upendo huku idadi ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu imeongezeka .
Mwita ameongeza kuwa, "Tuendeleze jitihada za mradi huu kuwaibua wale wote wenye mahitaji maalum,tusiwaache na kuwafungia ndani kwani wana haki kama yalivyo makundi mengine katika jamii.”
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Taasisi ya Shule Direct katika mradi wa elimu jumuishi Dainess Mollel ameeleza kuwa mradi huo wa pamoja katika elimu jumuishi ni ambao unatekelezwa na nchi tatu ambayo ni Tanzania,Kenya na Malawi na kwa Tanzania ipo chini ya Taasisi ya Shule Direct ambayo imechukua jukumu la kubeba mradi wa pamoja.
Aidha Dainess amewataka wanajamii kuendeleza jitihada za kufanya uchechemuzi bila uwepo wa shule direct.
"Ninyi kama jamii kwa uwezo wenu wa mmoja mmoja mnaweza kusimama msitari wa mbele kuendelea kuwatetea watoto wetu wenye mahitaji maalum na kuendelea kuboresha utekelezaji wa Mazingira ya watoto wenye mahitaji maalum"ameeleza.
Mradi huo ulianzishwa mwaka 2022 kwa mkoa wa Dodoma,Mwanza na Dar-salaam ili kuboresha uchechemuzi kwa uwekezaji kwenye maswala ya msingi ya elimu jumuishi katika jamii.
No comments:
Post a Comment