WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO KUNUFAIKA NA MIKOPO YA BIL. 18.5 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 6, 2024

WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO KUNUFAIKA NA MIKOPO YA BIL. 18.5


Na WMJJWM, Dar Es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imetenga Sh. Bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara ndogondogo nchini kwa riba nafuu kupitia benki ya NMB.

Hayo yamebainika wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya miaka miwili kati ya Wizara hiyo na Benki ya NMB iliyofanyika Mei 6, 2024 jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akishuhudia tukio hilo, amesema kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Serikali imechukua hatua kuhakikisha inaimarishwa ikiwemo kuwapa fursa ya kupata mikopo ya kuwawezesha kuinuka kiuchumi.

"Tukumbuke nia ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ustawi wa wafanya biashara ndogo ndogo ilianza tangu 2022 alipounda Wizara na kuweka kundi hili kwenye Wizara hii. Aidha, alitoa fedha ya kujenga ofisi za Machinga kila mkoa na kuelekeza wapewe maeneo. Hivi sasa mikoa 9 imekamilisha ujenzi wa ofisi na mingine ofisi ziko hatua mbalimbali za ujenzi." amesema Waziri Dkt. Gwajima.


Waziri Dkt. Gwajima amewataka wote watakaokopeshwa fedha hiyo wajue kuwa watatakiwa kurejesha pamoja na riba kidogo ambayo imewekwa ili kusaidia usimamizi na uendelevu na kufanya mkopo huu utakuwa na tija na hatimae wafanyabiashara wengi watafikiwa na kunufaika.

Ameongeza pia fedha hiyo itakuwa chachu ya kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Naye Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amesema Serikali imeshaweka utaratibu wa kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo nchini kote.

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amebainisha kuwa,
NMB itawatembelea wafanyabiashara ili kujiridhisha
na kujua mahitaji yao, vilevile watatoa elimu ya kifedha kwa lengo la kuwawezesha kuwa na nidhamu ili kutimiza malengo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga, SHIUMA John Lusinde ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo akisema 
wamekuwa wakipata shida ya mikopo kuwa na riba kubwa na benki nyingi kuwa na wasiwasi wa kurejeshwewa fedha zao.

 Amemshukuru Rais Samia kwa kuyajali makundi mbalimbali na kuahidi kuhakikishwa viongozi wa SHIUMA wanawahamasisha kurudisha kwa uaminifu.

No comments:

Post a Comment