|
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Babati iliyopo Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, wakifuatilia filamu ya mafunzo ya elimu ya fedha, yenye maudhui mbalimbali ikiwemo madhara ya kukopa bila malengo, madhara ya kukopa sehemu ambazo hazijasajiliwa, kuweka fedha kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa, matumizi mabaya ya fedha binafsi na mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa fedha, mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha, kwakuwa wanafunzi hao ni miongoni mwa watumiaji wa huduma za fedha na mabalozi kwa wazazi wao kutokana na elimu ya fedha waliyoipata. |
|
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akikabidhi nyenzo ya kufundishia kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, Bw. David Malisa, kwa ajili ya kwenda kutoa elimu hiyo kwa baadhi ya wanakijiji wenzake ambao hawajafika kupata mafunzo hayo katika shule ya msingi Osterbay kutokana na changamoto mbalimbali. |
|
Baadhi ya wajasiriamali na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Mkoani Manyara, wakiendelea kufuatilia mafunzo ya elimu ya fedha katika shule ya msingi Babati iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara, kwa njia ya filamu yenye maudhui mbalimbali ikiwemo madhara ya kukopa bila malengo, madhara ya kukopa sehemu ambazo hazijasajiliwa, kuweka fedha kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa, matumizi mabaya ya fedha binafsi na mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa fedha, mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha na kutolewa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI. |
|
Mmoja wa washiriki wa Elimu ya fedha katika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, Bw. David Malisa, akivaa tisheti yake yenye ujumbe wa “Elimu ya Fedha Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi”, aliyokabidhiwa na Afisa Maendeleo ya jamii Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bi. Avelina Kapologwe, baada ya kufaulu kuelezea kwa ufasaha maudhui yote yaliyopo kwenye filamu ya mafunzo ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na kuahidi kwenda kuwapa elimu hiyo wanakijiji wenzake ambao hawajahudhuria kupata elimu ya fedha kutokana na changamoto mbalimbali. |
|
Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa elimu ya fedha kwa baadhi ya Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, ambapo mafunzo hayo kwa Mkoa huo awamu hii ya kwanza yalianza katika Halmashuri ya Wilaya ya Mbulu, huku vijiji mbalimbali vya mkoa wa Manyara vikitarajiwa kufikiwa na watumishi wa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ili kuwapa wananchi elimu ya fedha. |
|
Picha za matukio mbali mbali ya mafunzo ya elimu ya fedha katika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi walio vijijini kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya Fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha-Manyara) |
Na Asia Singano, WF, Manyara.
Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuendelea kuwapatia elimu ya fedha kutokana na faida walizozipata baada ya kutembelewa na watumishi wa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI na kupatiwa elimu hiyo ya fedha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupatiwa elimu hiyo katika shule ya Msingi Osterbay, wananchi hao wamesema kuwa, hapo awali hawakuwa na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha wanazozipata hali iliyosababisha wandelee kudidimia kiuchumi kutokana na matumizi mabaya ya kipato chao.
‘’Tunaomba Wizara ya Fedha, itoe elimu hii mara kwa mara kwa watu wote nchini” Alisema Bi. Anthonia Anthon.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Osterbay, Mwl. Walter Ulotu, alisema kuwa elimu hiyo ya fedha itawasaidia watumishi wa umma hususani walimu wa shule hiyo waliopata fursa ya kushiriki katika mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha.
‘’Nimeona wajasiriamali ni wengi ambao wamehudhuria mafunzo haya kwahiyo tunaipongeza Wizara ya Fedha, lakini pia kwa kuwa yamefanyika hapa shuleni imeweza kutoa fursa kwa baadhi ya walimu wangu kujipatia elimu ya ujasiriamali na kuweka akiba na matumizi sahihi ya fedha binafsi’’ Alisema Mwl. Ulotu.
Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa elimu ya fedha ni vyema Wizara ya Fedha ikaendelea kutoa elimu hii ili kuwasaidia wananchi kuelewa masuala mbalimbali ya kifedha ikiwemo kuweka akiba na matumizi bora ya fedha na kuandaa maisha ya kustaafu pamoja na maisha ya uzeeni.
‘’Pamoja na mambo mengine lakini nimefurahia mada ya kujiandaa kustaafu, wengi wanakosa ile elimu ya fedha kwahiyo kiinua mgongo wanachokipata wanapostaafu hutumia vibaya, wengine hukimbilia kununua vyombo vya usafiri, ingependeza elimu hii itolewe mara kwa mara ‘’ Aliongeza Mwl. Ulotu.
Naye Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa Wizara ya Fedha itahakikisha kuwa elimu ya fedha inawafikia Watanzania wote waliopo mjini na vijijini ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu masuala ya fedha.
‘’Tunaendelea na programu hii katika mikoa mingine yote Tanzania, kwa awamu mbalimbali, lakini kwa awamu hii tulifanya kwa mikoa nane, lakini programu hii ni endelevu si kwa mwaka huu pekee, kila mwaka tutakuwa tunaendelea, lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na elimu ya fedha na wanapata uelewa wa kutosha katika kufanya maamuzi sahihi ya kutumia huduma sahihi za fedha’’ Alisema Bw. Kimaro.
Elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya Mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi walio Vijijini ili kuwaongezea uelewa wa masuala ya Fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha.
No comments:
Post a Comment