Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amezitaka benki na taasisi za fedha nchini kuandaa bidhaa na huduma zinazolenga wachimbaji na wadau wengine wa sekta ya madini, akisema hatua hiyo itasaidia kuchochea ukuaji wa sekta hiyo na uchumi kwa ujumla.
Gavana Tutuba ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dk Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Amesema sekta ya madini ina nafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania, hivyo taasisi za fedha zinapaswa kuona fursa zilizopo katika sekta hiyo na kuandaa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.
“Nimepita katika mabanda ya benki mbalimbali katika maonesho haya na nimeona wameanzisha bidhaa zinazowalenga wachimbaji wa madini na wadau wa sekta hii kwa ujumla.
“Hata hivyo, nitoe rai kwa wale ambao bado hawajaanzisha bidhaa kwa ajili ya wachimbaji kufanya hivyo, kwa sababu sekta hii ni fursa na ina mchango mkubwa katika uchumi wetu,” amesema.
Gavana Tutuba amesema taasisi za fedha hazipaswi kuiona sekta ya madini kwa mtazamo wa vihatarishi pekee, bali zinapaswa kutafuta namna ya kuvirasimisha na kuvitumia fursa zilizopo ili kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji.






No comments:
Post a Comment