TARURA NJOMBE YAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 3, 2026

TARURA NJOMBE YAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA


‎Na Mwandishi Wetu - Njombe
‎

‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Njombe inaendelea na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara inayolenga kuboresha usafiri, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
‎
‎Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Meneja wa TARURA wilaya ya Njombe, Mhandisi Costantine Ibengwe amesema Wakala umejipanga kuhakikisha miradi yote iliyopangwa inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati kwa kuzingatia masharti ya mikataba.
‎
‎Amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya Igeleke–Matalawe yenye urefu wa kilomita 1.16 kwa kiwango cha lami mradi unaolenga kuboresha kwa kiasi kikubwa usafiri na mawasiliano katika eneo hilo.
‎
‎"Mradi huu ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambapo unajumuisha ujenzi wa boksi kalavati pamoja na uwekaji wa taa za barabarani", amesema.
‎
‎Katika hatua nyingine, Mhandisi Ibengwe amesema TARURA Wilaya ya Njombe imeendelea kuchukua hatua za maandalizi ya kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha ikiwemo kuboresha na kusafisha mifereji ya maji katika maeneo mbalimbali.
‎
‎Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha maji ya mvua yanaelekezwa katika njia sahihi na kupunguza uwezekano wa maji kuingia kwenye makazi ya wananchi huku miundombinu ya barabara ikiendelea kuwa katika hali nzuri.
‎
‎Kwa upande wake, Bw. Frank Mtewa mkazi wa Mji wa Njombe amesema ujenzi wa barabara ya Igeleke–Matalawe ni hatua muhimu kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kila siku.
‎
‎"Barabara hii imekuwa changamoto kwetu lakini ikikamilika tutaweza kupita kwa urahisi zaidi hata wakati wa mvua", amesema.
‎
‎Utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea katika maeneo mbalimbali wilayani Njombe huku TARURA ikiendelea kuimarisha miundombinu ya barabara kwa lengo la kuwezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa kwa urahisi pamoja na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa usalama katika misimu yote.

No comments:

Post a Comment