Watoa huduma za fedha mkoani Manyara wametakiwa kufuata sheria na taratibu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwemo kujisajili, kutoza viwango sahihi vya riba na kuwapa nakala za mikataba wakopaji baada ya wao kuelewa mkataba wa makubaliano ya kukopa na kusaini ili kuepuka adhabu mbalimbali zitakazotolewa kwa wanaokiuka sheria za huduma za fedha.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga, ofisini kwake alipokutana na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha kabla hawajaingia kwenye kikao cha Baraza la Biashara lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kutoa elimu ya fedha kwa wajumbe wa kikao hicho.
Alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya uchunguzi kuwabaini wanaofanya biashara ya kutoa huduma za fedha bila leseni, ambapo baadhi yao wamekuwa wakikamatwa na kuadhibiwa huku akiwaonya wafanyabiashara wasiofuata kanuni, taratibu na sheria ya huduma za fedha kusajili biashara zao kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
‘’Wafanyabiashara wanaofanya biashara zao bila kujisajili, bila kufuata sheria, waache na Serikali ipo kazini tumekuwa tukiwakamata na tutaendelea kuwakamata na sheria itachukua mkondo wake’’ Alisema Bi. Sendiga.
Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha katika mkoa wake kutokana na mkoa huo kuwa na uhitaji mkubwa wa elimu ya fedha, kwakuwa wananchi wengi wamekuwa wakijiingiza kwenye mikopo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu na baadae kusababisha umasikini.
‘’Kwanza nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wizara ya Fedha, kupitia Hazina kwa kuja na mpango huu mzuri wa kutoa elimu ya fedha, maeneo makubwa ambayo wanaathirika ni pamoja na watumishi wa Umma na wafanyabiashara wadogowadogo, sisi kama Mkoa tuna changamoto hiyo pia kwa baadhi ya wananchi wetu’’ Alisisitiza Bi. Sendiga.
Kwa upande wake Mwl. Hamisi Maginga mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, alisema kuwa kukosa elimu ya fedha kumechangia baadhi ya walimu kujiingiza kwenye mikopo mingi iliyosababisha baadhi yao kupata msongo wa mawazo kutokana na kuwa na mikopo iliyokithiri kutoka kwenye taasisi zenye riba kubwa.
“Tumekuwa na tatizo kubwa sana hasa kwenye sekta yetu ya elimu, walimu wamekuwa na tabia ya kuwa na mikopo mingi, mpaka inafikia hatua hawawezi kuhimili mahitaji ya familia zao, na wengine imefikia hatua mpaka kadi zao za benki zinabaki huko kwa taasisi za fedha’’ Alisema Mwl. Maginga.
Naye Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa Wizara ya Fedha itahakikisha kuwa elimu ya fedha inawafikia wananchi wote kutokana na umuhimu wa elimu hiyo.
“Lengo la program hii ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafikiwa na kupewa elimu ya fedha, na chimbuko lake ni baada ya utafiti mdogo kufanyika na kubaini kwamba wananchi hawana uelewa mkubwa na wa kutosha wa elimu ya fedha na hivyo wanaendelea kusaidiwa kwa kila hali, kupewa mikopo na hawajikwamui kumbe wanachokosa ni elimu ya fedha’’ Alisema Bw. Kimaro.
Wizara ya Fedha ilianza kutoa elimu ya fedha katika maeneo ya Mijini kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi walioko Vijijini kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa masuala ya fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha.
No comments:
Post a Comment