Na Ofisi ya Rais TAMISEMI
Maafisa Viungo (Focal persons) wa Ilani wa Mikoa Tanzania Bara wametakiwa kukamilisha na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM kupitia Mfumo wa Dashboard ifikapo Julai 15, 2024.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta wakati akifunga mafunzo na kikao kazi kwa Maafisa Viungo wa Ilani wa Mikoa Tanzania Bara tarehe 7 Juni, 2024 katika Manispaa ya Singida mkoani Singida ambapo aliwaagiza Maafisa hao kukamilisha taarifa hiyo ya Ilani kwa usahihi, ubora unaokusudiwa na kuziingiza kwenye mfumo na kuwasilisha kwa wakati.
“kwa kuwa kipindi hiki tunaendelea na maandalizi ya mpango kazi na taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2024, nitumie fursa hii adhimu kusisitiza kuwa taarifa za utekelezaji wa Ilani za Mikoa kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2024 zikamilishwe na kuwasilishwa kupitia mfumo wa Dashboard ifikapo tarehe 15 Julai, 2024” alisema Bi. Kimoleta.
Aliongeza kuwa , kueasilisha taarifa hizi kwa wakati zitatoa nafasi kwa ngazi za juu kuchambua, kuhakiki na kuandaa taarifa jumuishi kwa umakini na kuwasilisha kwa viongozi ikiwa na ubora unaotarajiwa.
Aidha, amewataka Maafisa hao kuhakikisha kuwa mikoa yao inaandaa vikao kazi na Maafisa Viungo wa Halmashauri zao ili kupitia viashiria vilivyopo na vinavyotakiwa kutekelezwa na Halmashauri ili kuwa na picha ya pamoja ya taarifa na viashiria vinavyotakiwa kuingizwa katika mfumo.
Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya mgeni rasmi Bw. Hekima Chengula Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu alisema Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo iliyopewa jukumu la kuratibu usimamizi wa Utekelezaji wa Ilani ya CCM Kitaifa ikishirikiana na Wadau wengine ikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI hivyo itahakikisha inazifanyia kazi changamoto za Mfumo wa Ilani ili watumiaji waweze kutimiza majukumu yao kwa wakati.
Akitoa neno la shukrani -Bi. Susana Ndunguru Mwenyekiti wa Maafisa Viungo wa Ilani Tanzania Bara ameeleza kuwa kikao kazo hiki kimekuwa na manufaa makubwa kwao na kuwa sasa wataandaa taarifa sahihi zaidi, zenye ubora unaotarajiwa na kuzitoa kwa wakati.
Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoandaliwa kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu yalikuwa na lengo la kuwajengea uwezo Maafisa Viungo wa Ilani wa Mikoa kupitia mpango kazi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 kwa kipindi cha Januari -Juni, 2024 yaliwahusisha Maafisa Viungo wa Ilani wa Mikoa 26, Maafisa Viungo wa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment