WATENDAJI SERIKALINI WATAKIWA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 8, 2024

WATENDAJI SERIKALINI WATAKIWA KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WANANCHI


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaagiza watendaji wa Serikali nchini kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Akizungumza leo Juni 8, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Katome, Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Biteko amesema ni wajibu wa watendaji wa Serikali kuhakikisha kero za wananchi zinapata ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawapatia wananchi maendeleo.

“Natumia jukwaa hili la Katome kuwaelekeza watendaji wote wa Serikali nchi nzima kuwafuata wananchi popote walipo kusikiliza kero zao na kuzitatua. Watanzania wanataka viongozi tujibu kero zao, na sisi tumeaminiwa na Chama cha Mapinduzi hivyo tufanye kazi kwa niaba ya Chama”, amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema “Waliotuchagua wametupa nafasi ya kuwaongoza tusiwe mabwana kwao tuwatumikie.”

Aidha, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kujiandaa na kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwachagua viongozi wenye maono ya kuwaongoza na kuwaletea maendeleo na si wale wanaowagawa wananchi kwa namna yoyote ile ikiwemo watoa rushwa.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanawaletea wananchi maendeleo kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.

“Katika mwaka wa fedha 2024/25 Mhe. Rais Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa njia nne katika barabara ya Mwanza - Nyegezi - Usagara – Kigongo Busisi kwa maneno yake alielekeza tujenge barabara ya njia nne ili kuunganisha na daraja la Kigongo - Busisi na hii itasaidia sana kutatua tatizo la foleni”, amesema Mhe. Bashungwa.

Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa daraja hilo na kusema kuwa ujenzi wake umefikia asilimia 85 na linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Katome, Mhe. Joseph Maganga ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi wa maji katika kata hiyo.

“Tumepata mradi mkubwa wa maji unaogharimu shilingi milioni 449 kwa sasa umekamilika na wananchi wameanza kunufaika na tuna vituo 13 na kaya 33 tayari wameunganishiwa maji kutoka katika vituo.” Amesema Mhe. Maganga.

No comments:

Post a Comment