MAJALIWA ATOA KAULI YA SERIKALI KUPINGA UKATILI WENYE UALBINO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 20, 2024

MAJALIWA ATOA KAULI YA SERIKALI KUPINGA UKATILI WENYE UALBINO


UTANGULIZI
   
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kushiriki katika kikao hiki cha 50 cha Mkutano wa 15 wa Bunge tukiwa na afya njema. 

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuungana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na wewe Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wenzangu na Watanzania wote, kutoa pole na salamu za rambirambi kufuatia kuondokewa na Mheshimiwa Dkt. Shogo Mlozi, Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki.


 Kama mtakumbuka, kifo kilitokea tarehe 13 Juni, 2024 katika Hospitali ya Mount Meru huko Arusha. Marehemu Dkt. Shogo Mlozi atakumbukwa kwa uthubutu, uzalendo na uwakilishi wake uliouheshimisha Taifa letu katika Bunge muhimu la Afrika ya Mashariki. 

Aidha, niungane na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kutoa salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Tickson Nzunda kilichotokea tarehe 18 Juni, 2024 kwa ajali ya gari. Marehemu Tickson Nzunda tutamkumbuka kwa utumishi wake ndani ya nchi yetu kupitia nafasi mbalimbali alizowahi kuhudumu iiwemo nafasi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge. Mwenyezi Mungu awapumnzishe marehemu wote kwa amani. Amina

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari, 2023 zimetoa fursa ya uwepo wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kwa siku ya Alhamisi. Vilevile, kanuni ya 44(4) imeruhusu Waziri Mkuu kutumia kipindi cha maswali ya papo kwa papo kutoa taarifa au ufafanuzi kuhusu suala lolote linalohusiana na shughuli za Serikali na lenye maslahi kwa umma. 

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninasimama mbele ya Bunge lako tukufu nikiwa na huzuni kubwa kutokana na matukio ya kikatili yaliyotokea hivi karibuni. 

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 31 Mei, 2024 kulitokea tukio la kutekwa kwa Mtoto Asiimwe Novati (mwenye Ualbino) mwenye umri wa miaka miwili na nusu mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Mulamula, Kata na Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera nyumbani kwao Kebyera.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 01 Juni, 2024 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Ofisi ya Rais TAMISEMI, walithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Mtoto huyo alikuwa na mama yake wakati walipovamiwa na vijana wawili majira ya saa 2:15 usiku ambapo mmoja alimkaba koo mama yake ambaye alikuwa nje ya nyumba na mwingine aliingia kwa haraka ndani na kumchukua mtoto na kutokomea naye kusikojulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 17 Juni, 2024 Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ilipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa Mkoa wa Kagera kuhusu kifo cha mtoto huyo ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa kwenye mfuko wa plastiki kando ya karavati pembeni mwa barabara itokayo Kijiji cha Ruhanga kwenda Kijiji cha Malele Kata ya Ruhanga. Sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa mauaji haya yameibua hisia ya maumivu yasiyoelezeka kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tukio hili linaelekea kufanana na tukio lingine lililotokea tarehe 4 Mei, 2024 ambapo mtoto Julius Kazungu (10) mwenye ualbino, mkazi wa Katoro, Geita, alivamiwa majira ya saa 2:00 usiku na mtu asiyejulikana ambaye alikuwa ameficha sura yake na kuanza kumkata na panga kichwani na mikononi. Mtoto huyo alilazwa na sasa anaendelea vizuri na Serikali ya Mkoa inagharamia matibabu ya mtoto huyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhai ni zawadi ya thamani isiyo na kifani, lakini kwa masikitiko makubwa, zawadi hii imekuwa ikitwaliwa kwa njia za kinyama na za kikatili kwa ndugu zetu wenye Ualbino kwa sababu ya imani potofu. Mauaji haya yameacha majonzi yasiyofutika mioyoni mwa Watanzania, yametuacha tukiwa na huzuni isiyopimika na kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu.

Hatua zilizochukuliwa na Serikali

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imelaani vikali vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino na kwa kuzingatia nia thabiti ya kukomesha tabia hiyo, Serikali imefanya yafuatayo: 

Uchunguzi ulianza mara baada ya tukio hilo.
Washukiwa tisa wa tukio la kutekwa na kuuawa mtoto Asiimwe wamekamatwa na Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi Mkoani Kagera linaendelea na upelelezi wa tukio hili.
Wataalam wa Ustawi wa Jamii wanaendelea kutoa huduma ya msaada wa kisaikolojia kwa waathirika kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya Mkoa wa Kagera na Halmashauri ya Wilaya ya Muleba; 

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa nitumie nafasi hii kuungana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole wa wazazi, ndugu, jamaa na Watanzania kwa tukio hilo ambalo limeleta simanzi kubwa kwa Watanzania wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na taharuki kubwa iliyotakana na tukio hilo, nimeona nitumie kipindi cha leo kwanza kwa kutoa pole, lakini pia kuwakumbusha Watanzania wote wajibu wao katika masuala ya ulinzi wa mtoto na usalama wa jamii nzima kwa ujumla. Vilevile, kutoa taarifa kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa makundi mbalimbali likiwemo kundi la watoto na jamii ya watu yenye ulemavu wakiwemo wenye Ualbino.

MASUALA YA ULINZI WA MAKUNDI YA WATU WENYE UALBINO

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa haki ya mtu kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kutoka kwa jamii, kwa mujibu wa sheria. Kwa msingi huo, watu wenye ualbino au ulemavu wa aina nyingine yoyote, wanalindwa na Katiba ya nchi. Haki zote zilizoainishwa kisheria kwa mujibu wa Katiba kwa Watanzania wote wakiwemo watu wenye ulemavu, wanastahili kuzifurahia. 

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukweli huo, ni jambo lisilokubalika kwa Mtanzania au mtu mwingine yeyote kuondoa haki hiyo ya kikatiba au haki zingine zinazotambuliwa na sheria au haki za kijamii. Kitendo chochote cha aina hiyo na vinavyofanana na hivyo havikubaliki na Serikali haiwezi kufumbia macho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uwepo wa dhana potofu zinazoambatana na ukatili na mauaji ya watu wenye ualbino zikiwemo tamaa ya kupata mali nyingi, utajiri, cheo au mafanikio ya aina yoyote. Naomba kulieleza Bunge lako tukufu kuwa, dhana hizo ni potofu na hazistahili kufumbiwa macho na jamii zetu na wananchi wote wana wajibika kushiriki kikamilifu katika kuyakemea matendo hao kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako tukufu lilitunga Sheria ya Uchawi, Sura ya 12 ya Mwaka 1998, ambayo inabainisha pamoja na mambo mengine kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote anayeshauri kuhusu matumizi ya uchawi au vifaa vyovyote vya kichawi. Pia, sheria inabainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote anayedhamiria kusababisha kifo, ugonjwa, madhara au msiba kwa jamii, mtu au kikundi cha watu. 

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya Sheria hiyo, Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 inaweka bayana kuwa ni kosa kisheria, kuteka, kutesa, kusababisha madhara au kuua mtu yeyote. 

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, Sheria ya Mtoto Sura ya 13, sambamba na katazo la mtoto kufanyiwa ukatili, unyama, vitendo visivyo vya kibinadamu au udhalilishaji unaohusisha matendo ya kimila yanayoondoa utu wa mtu au kuathiri ustawi wa akili au maumbile yake, inatoa wajibu kwa Serikali za Mitaa kulinda na kutetea maslahi ya mtoto ili kuhakikisha analelewa kwenye mazingira stahiki na kwa maadili ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kuwa utendaji wa makosa ya kuteka, kunyanyasa au kuua Watoto, walemavu, na Watu wenye Ualbino, hayatokani na ombwe la sheria zetu. Makosa haya yanatokana na tamaa kama nilivyoeleza hapo juu.

JITIHADA ZA SERIKALI KATIKA KUIMARISHA MASUALA YA ULINZI NA USALAMA WA MAKUNDI MBALIMBALI KATIKA JAMII

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kuhakikisha masuala ya ulinzi na usalama wa makundi mbalimbali katika jamii. Kama tunavyofahamu masuala haya ni mtambuka na ufanisi wake unahitaji ushiriki wa wadau wote muhimu zikiwemo Wizara za kisekta, Sekta Binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Kimataifa na jamii kwa ujumla. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wadau hao wanahusika katika kutekeleza Sera, Sheria, Miongozo, Programu na mikakati ili kuimarisha mfumo wa ulinzi na usalama wa makundi mbalimbali katika jamii. 

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuimarisha mifumo hiyo, Serikali pia imeendelea kutekeleza matakwa ya Itifaki na Mikataba ya kikanda na kimataifa inayolenga kuimarisha mfumo wa utoaji haki; kutoa huduma kwa makundi mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu wajibu wa kila mwananchi katika masuala ya ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika, Serikali imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na afua mahsusi ili kuhakikisha matakwa hayo ya kisheria yanasimamiwa kikamilifu. Hatua hizo zimekuwa zikitekelezwa ili kuhakikisha makundi yote katika jamii yanaishi kwa amani, utulivu na furaha pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya ukiukwaji wa sheria ikiwemo kutoa adhabu kali kwa wote wanaobainika kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto, watu wenye ualbino, wanawake pamoja na makundi mengine.

Katika hatua nyingine Serikali imeendelea kutoa elimu na kushirikisha jamii katika masuala ya ulinzi pamoja na kuweka mifumo thabiti katika ngazi mbalimbali. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na zifuatazo: 
Kuboresha mifumo ya kisheria ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto kwa kufuata Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Kanuni za ulinzi wa Mtoto za Mwaka 2015 na Mfumo wa Taifa Jumuishi wa Usimamizi wa Mashauri ya Watoto, Katika kuwahudumia watoto wanaohitaji ulinzi na usalama.

Kuanzisha Mfumo wa Taarifa Jumuishi wa kitaifa wa kushughulikia Mashauri ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi nchini (NICMS 2017). Hadi Aprili, 2024, jumla ya watoto 708,957 (ME 340,661, KE 368,296) wanaoishi katika mazingira hatarishi wametambuliwa katika Halmashauri zote nchini na kupatiwa huduma kulingana na mahitaji yao;

Kuanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Halmashauri zote 184 zimepewa jukumu la kutoa elimu, kulinda na kutoa taarifa kuhusiana na ukatili; 

Kuanzisha Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia Ukatili wa Watoto Mtandaoni Pamoja na kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni, tarehe 10 Februari, 2024 Jijini Dodoma wadau zaidi ya 460 walishiriki. Lengo la kampeni hiyo ni kuelimisha watoto, wazazi, walezi, walimu, viongozi wa dini, viongozi wa Taasisi zisizo za Serikali, Wizara za kisekta, na jamii kuhusu kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili mitandaoni sambamba na ukatili wa aina nyingine.

Kuanzisha Dawati la Ulinzi na Usalama wa Mtoto Ndani na Nje ya Shule. Jumla ya madawati 617 katika Shule za Sekondari na Msingi katika Mikoa 10 Tanzania Bara yameanzishwa hadi Desemba, 2022. Madawati haya yameundwa sambamba na mabaraza ya watoto 377 katika Shule za Msingi na Sekondari; 

Kuanzisha Nyumba Salama kwa ajili ya kuhudumia Wahanga wa ukatili. Jumla ya Nyumba salama 16 katika mikoa 9 ya Tanzania Bara zimeanzishwa hadi kufikia Aprili 2024; 

Kuanzisha Simu ya Bure ya Msaada namba 116 ambayo hutumika kutoa taarifa za vitendo vya ukatili katika jamii. Kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya simu 240,657 kuhusu watoto zilipokelewa na kupatiwa huduma;

Kutoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi/walezi na vikundi vya malezi. Elimu hii pia ilitolewa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa, redio jamii, mikutano ya hadhara na kwenye nyumba za ibada. Lengo ni kuwawezesha wazazi/walezi kuzuia vitendo vya ukatili katika familia;

MIKAKATI YA ULINZI WA WATU WENYE UALBINO

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha watu wenye ualbino wanalindwa kama ifuatavyo:- 

Serikali inaandaa Mpango wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino (NAP) kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) na Wadau; 

Serikali inaandaa kikao cha Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara kitakachofanyika tarehe 03 Julai, 2024 kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa watu wenye ualbino;

Kutoa elimu ya ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wakiwemo Watu wenye Ualbino kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Elimu Maalum wa Mikoa yote nchini;

Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na kuandaliwa kwa Mkakati wake wa Utekelezaji wa Miaka Mitano (National Five Year Implementation Strategy 2024/2025- 2029/2030) na Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miaka Mitano ambayo itazinduliwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025;

Kukamilisha na kuzindua Mkakati wa miaka mitatu 2024-2027 wa Upatikanaji wa Teknolojia saidizi kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino, mkakati huu umepangwa kuzinduliwa mwezi Julai, 2024; 

Kuandaa na kukamilisha Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu 2024/2025 2026/2027;  

Kuendelea na ubainishaji na usajili wa watu wenye ulemavu ngazi za kijiji na mtaa kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki na Kanzidata ya Watu wenye Ulemavu niliouzindua Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani tarehe 02 Desemba, 2023 jijini Dodoma. 

Kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu. 

MAELEKEZO

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha uliopo, vitendo vya mauaji ya albino vinahusisha mtandao wa watu na siyo mtu mmoja mmoja tu. Isitoshe, kutokana na maelezo yaliyotangulia, ni dhahiri kwamba tayari Serikali imeshajenga mifumo thabiti ya udhibiti na suala lililobaki ni upande wa ushiriki wa makundi yote ya jamii katika kuhakikisha vitendo hivyo viovu vinakomeshwa hapa nchini. 

Hivyo basi, kwa kutambua jukumu tulilonalo kama Taifa nitumie nafasi hii kuyataka makundi na taasisi mbalimbali katika jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo vya ukatili. 

 WAJIBU WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
 
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuzuia unyanyasaji na mauaji ya watu wenye ualbino, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zinawajibika katika usimamizi, ulinzi na utoaji wa huduma kwa watu wenye ualbino. Hivyo basi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya hakikisheni kila halmashauri inaanzisha Operesheni Maalum za Ulinzi kwa watu wenye ualbino. Operesheni hizi zihusishe vikosi vya usalama ili kuhakikisha ulinzi wa watu wenye ualbino dhidi ya mashambulizi na vitisho. 

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka za Mikoa na Wilaya zihamasishe ushiriki wa jamii katika kuhakikisha ulinzi na haki za watu wenye ualbino. 

WAJIBU WA WAZAZI NA WALEZI

Mheshimiwa Naibu Spika, wazazi wanao wajibu kwa watoto wao. Wajibu wa wazazi kwa watoto wao ni kuwapa malezi bora yatakayowawezesha kuinukia kuwa watu wema katika jamii ambayo wataweza kuitawala dunia. Malezi hayo yanahusu yale yote anayofanyiwa mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama hadi anapofikia umri wa kujitegemea. Wazazi wote wawili, yaani baba na mama, wanahusika kwa ukamilifu na malezi haya. 

WAJIBU WA VIONGOZI WA MADHEHEBU YA DINI

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na wajibu wa wazazi na walezi, naomba nitumie fursa hii pia kusisitiza majukumu ya viongozi wa dini kwenye suala la kukemea maovu yanayotendeka kwenye jamii yetu hususan vya kuuawa kwa watu wenye ualbino nchini kunaonesha upotofu wa maadili na kukosa hofu ya Mungu. Vitendo hivyo vinapaswa kukemewa kwa nguvu na nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wetu wa dini tuungane pamoja katika kupambana na mauaji haya ya watu wasiokuwa na hatia hata kidogo. Hivyo, niwasihi watumie majukwaa yao ya ibada kuwahubiria waumini wao kuachana na vitendo hivyo vya ukatili ambavyo hata Mwenyezi Mungu anavikataza. Watu wenye ualbino wana haki ya kuishi kama walivyo watu wengine. 

WAJIBU WA WAGANGA WA JADI

Mheshimiwa Naibu Spika, waganga wa jadi wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wao katika mapambano na vita hii ya kuwalinda ndugu zetu wenye ualbino. Hivyo basi, ni wajibu wao kushiriki kukemea vitendo hivi vya mauaji na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuthamini maisha ya kila mtu, bila kujali hali ya maumbile yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwasisitize waganga wa jadi nchini kote washiriki kikamilifu katika kampeni za kupinga mauaji ya watu wenye ualbino. Wakati umefika kwenu nyote kushirikiana na Serikali katika kutokomeza imani potofu zinazochangia mauaji haya. Ninawasihi sana elezeni wazi kwamba hakuna tiba wala mafanikio yanayoweza kupatikana kwa kutumia viungo vya watu wenye ualbino. Badala yake, matendo haya yanavunja haki za binadamu na kumomonyoa utu wetu kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lifanye usajili wa waganga wa jadi na vituo vyao sambamba na aina ya huduma wanayoitoa kwa wateja wao ili kuweza kudhibiti huduma holela isiyofuata misingi ya utu na haki za binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (CHAWATIATA) kiwakatae na kuwatenga waganga wanaotumia njia za imani potofu, ramli chonganishi ikiwemo kutoa masharti ya kufanya mauaji ya watu wenye ualbino ili kufanikisha mahitaji ya wateja wao. Vilevile, toeni taarifa kwa mamlaka husika ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao. 

WAJIBU WA VIONGOZI WA KIMILA

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kuwa viongozi wetu wa kimila wana nafasi kubwa sana na wamekuwa nguzo muhimu katika jamii zetu kwa karne nyingi. Viongozi hawa wanaheshimika na kusikilizwa na wanajamii na wanao uwezo mkubwa wa kuhamasisha na kuongoza mabadiliko. Kwa kutambua nafasi yao ya pekee, ninawasihi viongozi wa kimila nchini kote, kutoka kila kona ya Tanzania, washiriki kikamilifu katika kukemea na kupinga mauaji ya watu wenye ualbino. 

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba viongozi wetu wa kimila wakiwemo Machifu washirikiane na Serikali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapopata fununu za mipango au vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino katika maeneo wanayoishi.  

WAJIBU KWA WANANCHI WOTE

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali, sote tunao wajibu wa kuwalinda watu wenye ualbino kwa kufichua njama zenye nia ovu na kutoa taarifa pindi tunapozibaini ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Vilevile, nitumie fursa hii kuwasisitiza wananchi waache tabia ya kufanya mizaha isiyo na staha hususan kuhusisha matumizi ya viungo vya watu, ama kuelezea kuwa viungo vya watu wenye ualbino vinaweza kuwaletea utajiri. Mizaha kama hii si tu inaonesha ukosefu wa heshima kwa watu wenye ualbino na familia zao, lakini pia inachochea ubaguzi na unyanyapaa. 

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa wito kwa Watanzania wote kuheshimu haki za binadamu na kuepuka kutumia lugha au kufanya vitendo ambavyo vinaweza kudhalilisha au kuumiza hisia za wengine. Ni wajibu wetu kama jamii kuhakikisha kuwa kila mtu anaishi katika mazingira salama na yenye heshima bila kujali tofauti zetu.

WAJIBU WA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na matukio ya aina hii ili yasiendelee kutokea, ninalielekeza Jeshi la Polisi kufanya yafuatayo:
Kuchukua hatua za haraka pindi linapopata fununu ya uwepo wa njama za utekaji na mauaji ya watu wenye ualbino. 

Kuendelea kufanya operesheni ya kuwakamata wote waliotajwa na watakaotajwa kuhusika kwenye matukio ya aina hii kwa lengo la kuua mtandao mzima wa wahalifu hawa na operesheni hizo ziwe endelevu. 

Polisi jamii ishirikishwe kikamilifu ili kupata taarifa zote muhimu katika maeneo husika na watoa taarifa wote walindwe ipasavyo. 

Kutumia taarifa za makazi na idadi ya watu wenye ualbino ili kuelekeza nguvu zaidi za ulinzi kwenye maeneo hayo. 

Kuendelea kufuatilia kutumia taarifa fiche zinazopatikana kutoka vyanzo mbalimbali. Hii itasaidia kubaini mipango inayopangwa na wahalifu ikiwemo wanaotafuta wateja wa biashara hizo na kuwabaini na kuwachukulia hatua kabla ya kutenda tukio.

Kufanya upelelezi kwa weledi ili kesi zinazopelekwa mahakamani ziwe na ushahidi wa kutosha.

Kutumia polisi kata kuhakikisha maeneo wanayoishi watu wenye ualbino yanatembelewa mara kwa mara ili kupata taarifa zao na kutambua mapema viashiria vyovyote ambavyo ni vya kihalifu pia kuwapa elimu namna ya kutambua mtu mwenye nia ovu na yule mwema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nielekeze Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kwa tukio hili la Kagera, mara baada ya upelelezi, wale watakaobainika wafikishwe mahakamani ili watuhumiwa waweze kuhukumiwa. Hii itasaidia kutoa fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya hivyo wakijua kuwa mkono wa sheria hautawaacha salama.

HITIMISHO

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa wabunge wenzangu kwa kushiriki kikamilifu katika kukemea vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino kupitia Bunge hili tukufu. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kushiriki katika kuongeza hamasa kuhusu elimu kwa wananchi katika maeneo yenu na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mipango ya Serikali kuhusu ulinzi wa jamii ya watu wenye ualbino.   

Mheshimiwa Naibu Spika, sote kwa pamoja yaani Serikali, mashirika ya dini, mashirika yasiyo ya Kiserikali, taasisi za haki za binadamu na Watanzania wote kwa ujumla tukae na tutafute njia muafaka itakayotumika kuelimisha jamii ili watu waachane na tabia hiyo mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ninaomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment