Yolanda Sánchez alikuwa ameripoti kupokea vitisho vya kuuawa na alikuwa ametekwa nyara mwaka jana
Watu wenye silaha wamemuua meya mwanamke wa mji mmoja nchini Mexico saa chache baada ya nchi hiyo kusherehekea kuchaguliwa kwa Claudia Sheinbaum kama rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo.
Yolanda Sánchez alipigwa risasi katika mji wa Cotija, ambao alikuwa ameutawala tangu Septemba 2021.
Alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kwenye wadhifa huo.
Ghasia dhidi ya wanasiasa zimegubika uchaguzi mkuu wa Mexico, ambao ulishuhudia wanawake wawili wakiwania kiti cha urais.
Yolanda Sánchez alivamiwa na watu wenye silaha katikati mwa Cotija, Michoacán, siku ya Jumatatu.
Vyombo vya habari nchini humo vinasema alipigwa risasi 19 na kufariki akiwa hospitali muda mfupi baada ya shambulio hilo. Mlinzi wake pia aliuawa katika mapigano ya bunduki.
Hakuna mtu aliyekamatwa kufikia sasa kuhusiana na shambulio hilo lakini inadhaniwa kuwa watu hao wenye silaha walikuwa wa kundi la uhalifu uliopangwa.
Bi Sánchez alikuwa ameripoti kupokea vitisho vya kuuawa baada ya kuchukua madaraka mnamo Septemba 2021.
Alizuiliwa kwa siku tatu na watu wenye silaha ambao walimkamata kwa mtutu wa bunduki wakati wa ziara ya jimbo jirani la Jalisco mnamo 2023.
No comments:
Post a Comment