Na Mwandishi Wetu,
Mbeya
Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) katika mwaka 2024 umetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 1.091 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za miradi ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri saba zinazotekeleza Mradi huo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Mbeya (Jumanne Juni 25, 2024) na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati wa siku ya pili ya kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa shughuli za mradi huo kwa mwaka 2024.
Dkt. Mapunda amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha inaweza mazingira wezeshi kwa wasimamizi wa ngazi zote za maamuzi zinazosimamia utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha fedha zilizotengewa zinawafikia kwa wakati ili kuweza utekelezaji miradi hiyo kwa wananchi.
Katika mwaka huu wa fedha tumepanga kutekeleza jumla ya miradi sita ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi fedha zake zitaanza kutolewa na kufikishwa katika Halmashauri zote zinazotekeleza miradiNawasihi tuweke jicho letu katika fedha hizo ili kuhakikisha zinatekeleza malengo yaliyokusudiwa amesema Dkt. Mapunda.
Aidha Dkt. Mapaunda ameitaja miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Malambo 3 katika Halmashauri za Wilaya za Mbarali, Wangingombe na Mpimbwe, Ujenzi wa Vitalu Nyumba katika Halmashauri za Wangingombe, Mbeya na Iringa, Ujenzi wa Kituo cha Kuchakata Maziwa katika Halmashauri za Wilaya ya Mbarali.
Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kuchakata mpunga katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, ujenzi wa kituo cha kuchakata asali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na ujenzi wa kituo cha kuchakata alizeti katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
Amefafanunua kuwa miradi hiyo imekusudia kuwawezesha wananchi kuachana na shughuli zisizo endelevu katika mazingira na hivyo kuwajengea uwezo wa kuendesha shughuli mbadala kwa ajili ya kujiongezea kipato katika maeneo yao.
“Mradi umepanga kuajiri Afisa Biashara ambaye kwa kushirikiana na Afisa Maendeleo ya Jamii wataweza kuwajengea uwezo wananchi kupitia vikundi vidogo vidogo ili kuendesha shughuli kwa mfumo wa kibiashara na kuuza mazao yao kwa ajili ya kujiongezea kipato amesema Dkt. Mapunda.
Ameongeza kuwa Serikali ilianzisha mradi huo mahsusi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki na mazingira ikiwamo ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa na uharibifu wa vyanzo vya maji na badala yake kuanzisha shughuli mbadala kwa ajili ya kuongeza kipato kwa wananchi.
Kikao kazi hicho kinahusisha Maafisa Viungo, Maafisa Mipango,Wahandisi wa Miradi, Maafisa Manunuzi, Maafisa Misitu na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Halmashauri za Wilaya zinazosimamia Mradi.
Mradi wa SLR unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 25.8 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano unaotarajia kukamilika mwaka 2025 ulioanza mwaka 2021 ukihusisha jumla ya Mikoa mitano, Halmashauri saba, Kata 18 na vijiji 54.
Halmashauri zinazonufaika na mradi huo ni Iringa Vijijini (Iringa), Wangingombe (Njombe), Wilaya ya Mbeya na Mbarali (Mbeya), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa) pamoja na Halmashauri za Wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).
No comments:
Post a Comment