Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imezifungia kampuni mbili kujihusisha na ununuzi wa umma kwa miaka 10 baada ya kubainika kuwa wameshiriki kufanya udanganyifu, huku kampuni moja ikijihusisha na kugushi nyaraka.
Kampuni hizo mbili zilizofungiwa miaka 10 kufanya manunuzi ya umma ni Kampuni ya Dacady Investment na High Winds Tanzania.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na PPRA, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Eliakim Maswi alieleza kuwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 10 ambayo imeanza Mei 21, mwaka huu hadi Mei 20, 2034 inajumuisha wakurugenzi, mawakala na washirika wa kampuni hizo.
“Kampuni hizo mbili zilifanya udanganyifu kwa kujiorodhesha kushindania zabuni moja wakati mmiliki wake ni mtu mmoja, jambo ambalo liliondoa ushindani wa haki,” alisema Maswi kwenye taarifa hiyo.
Alisema makosa ya aina hiyo hupelekea mtu mmoja kushinda zabuni tofauti kwa kutumia majina mbalimbali kinyume na taratibu za ununuzi, jambo ambalo linaathiri mchakato wa zabuni.
Aliongeza kuwa PPRA imeiongezea adhabu ya kifungo cha miaka mitatu Kampuni ya High Winds Tanzania kwa kushindwa kutekeleza mkataba wa ununuzi namba 014/2020/2021/PR/G/26 kati yake na Wizara ya Mambo ya Ndani, ambapo adhabu hizo mbili zitatekelezwa kwa pamoja.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA ameeleza kuwa Mamlaka hiyo imeifungia Kampuni ya Deaver PVC kushiriki kwenye michakato ya ununuzi wa umma kwa miaka 10 kuanzia Mei 21, 2024 hadi Mei 20, 2034, baada ya kubainika kuwa ilighushi nyaraka za makubaliano maalum (Framework Agreement) Na.0068009.
Alisema kampuni hiyo ilighushi makubaliano ya mfumo na kuyawasilisha katika chuo cha magereza Kiwira.
Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 102 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma, 2013, uamuzi wa PPRA kuzifungia Kampuni za Dacady Investment, High Wind Tanzania Company Limited na Deaver PVC Company Limited imeathiri mikataba ya ununuzi ambayo imeingiwa na taasisi za ununuzi na kampuni hizo kabla ya kutangazwa kwa tarehe ya uamuzi huo wa kuzifungia.
No comments:
Post a Comment