PROF. KUSILUKA "UBUNIFU NI AJIRA SIYO KUJIFURAHISHA'' - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 21, 2024

PROF. KUSILUKA "UBUNIFU NI AJIRA SIYO KUJIFURAHISHA''


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewataka Vijana nchini kupitia Bunifu mbalimbali walizonazo kujikita katika kutengeneza ajira badala ya kubaki kujifurahisha pekee.


Wito huo umetolewa  leo Juni 21,2024 jijini Dodoma na Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Lughano Kusiluka   wakati akifungua wiki ya Utafiti na Ubunifu kwa Mwaka 2024 yaliyoandaliwa Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu ya chuo hicho ambapo amesema lengo ni kuona Bunifu kutoka chuo hicho zikiuzwa nje ya nchi.


Kusiluka amesema amekuwa akivutiwa na uhodari wa wanafunzi wa chuo Kikuu cha Dodoma kwa ubunifu na maarifa yao ambayo ndiyo sababu ya kufanya vizuri katika mashindano ya TEHAMA ndani na nje ya nchi.


Amesema lengo la Chuo Kikuu cha Dodoma ni kuhakikisha kila mwanafunzi na mfanyakazi wa chuo hicho chini ya ndaki ya Sayansi za Kompyuta na elimu angavu anao uwezo wa kuonyesha ubunifu.


“Hatubuni kwasababu tunajifurahisha, akili mnemba hii sasa hivi tunainunua na vitu vyote tunavyotumia tunavinunua kutoka kwa watu ambao walibuni, lengo letu sasa na sisi tufike mahali tuwe na ujasiri wa kwamba hatuwezi kununua vitu kwasababu tunaweza kubuni na kutengeneza,”


“Na sisi tufike mahali tuseme hatutangoja China ifanye, hatutangoja Marekani, Ujerumani, Korea, Singapore wafanye kitu ndio sisi tukakifanye, hakuna mahali ambapo nimewahi kusoma kuwa akili za wale walioko kule zinatofautiana na za kwetu.” amesema Kusiluka.


Amesema watanzania wanatakiwa kuwa na ujasiri pamoja na uhakika wa kutengeneza bidhaa ambayo nchi za nje watakuwa na uwezo wa kuinunua kwani ubunifu ni fursa moja wapo ya kujipatia kipato.


Aidha ameongeza kuwa viongozi wa nchi wamekuwa wakisisitiza kuwa vyuo vikuu vinatakiwa  kuzalisha vijana ambao wakimaliza masomo wanakuwa na uwezo wa kujitegemea na kujitengenezea ajira.



Kwan upande wake Kaimu Rasi wa Ndaki hiyo Dkt. Daniel Ngondya amesema kupitia maonyesho hayo wanapata fursa ya kuonyesha jamii yale ambayo wanafunzi wa UDOM wanavyojifunza na kuweza kuyatenda kwa vitendo.


Amesema pia maonyesho hayo ni fursa ambayo inawezesha wanafunzi kukutana na wadau pamoja na wateja watarajiwa wa bidhaa za ubunifu pamoja na kubadilisha mtizamo uliokwepo kwa muda mrefu.


Wiki hiyo ya Ubunifu na Tafiti ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu yenye kaulimbiu `Kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu wa kidijtali’ imezinduliwa leo Juni 21,2024 na prof Lughano Kusiluka katika viwanja vya Nyerere Square.






No comments:

Post a Comment