SERIKALI YAHAMASISHA WAKULIMA KUTUMIA NJIA MBADALA YA MATUMIZI YA MADAWA KWENYE UZALISHAJI WA KAHAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 21, 2024

SERIKALI YAHAMASISHA WAKULIMA KUTUMIA NJIA MBADALA YA MATUMIZI YA MADAWA KWENYE UZALISHAJI WA KAHAWA

 


Na Saida Issa, Dodoma 


IMEELEZWA kuwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya soko la kahawa inayozalishwa kwa teknolojia ya kilimo hai (Organic coffee) ambayo hupelekea wakulima kupata bei nzuri katika soko, Serikali inahamasisha wakulima kutumia njia mbadala ya matumizi ya madawa kwenye uzalishaji wa kahawa. 


Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Moshi Vijiji Prof Patrick Ndakidemi alipouliza Je, ni lini Serikali itarejesha utoaji wa ruzuku ya pembejeo za dawa kwa Wakulima wa Kahawa?


Naibu huyo alisema kuwa Njia hizo ni pamoja na kupanda miche chotara ambayo inazalishwa na kusambazwa bure na Bodi ya Kahawa Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).


"Aidha, miche ambayo inazalishwa na kusambazwa kwa wakulima ina ukinzani na magojwa makuu ya kahawa ya chole buni na kutu ya majani ambayo ndiyo yaliyokuwa yanasababisha mahitaji ya matumizi makubwa ya madawa, 


Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2023/2024, jumla ya miche 21,899,560 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima wa kahawa katika mikoa yote inayozalisha kahawa nchini,"alisema. 


Alieleza kuwa Kati ya miche hiyo, mkoa wa Kilimanjaro ulipata miche 1,664,635 ambayo imesambazwa kwa wakulima ambapo, Wilaya ya Moshi imepata jumla ya miche 328,110 na kusambazwa kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika.

No comments:

Post a Comment