WANANCHI SENGEREMA WAASWA KUZINGATIA MATUMIZI YA VIZIMBA ILI KUEPUKA MADHARA YA MAMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 8, 2024

WANANCHI SENGEREMA WAASWA KUZINGATIA MATUMIZI YA VIZIMBA ILI KUEPUKA MADHARA YA MAMBA


Na Beatus Maganja

Wananchi waishio kandokando ya ziwa Victoria wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wamesisitizwa umuhimu wa kuzingatia matumizi ya vizimba vilivyojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake za TAWA na TAWIRI maalumu kwa ajili ya kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori aina ya mamba.

Hayo yamesemwa Juni 07, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Asenyi Ngaga alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika ziara iliyofanywa na Maofisa wa TAWA wilayani humo.

Mhe. Asenyi amesema licha ya Serikali kujenga vizimba hivyo kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wananchi kuishi kwa mazoea huku wakipuuzia kutumia vizimba hivyo na kuwataka wananchi hao kuacha tabia ya mazoea na kuchukua tafadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.

"Hatupendi kuona watu wanapotea ndio maana tunawakumbusha wananchi wetu kuendelea kuchukua tafadhali...Sasa changamoto ninayoiona kwa wananchi wa Sengerema hasa wanaoishi maeneo ya visiwani kwa kiasi kikubwa ni hali ya kuishi kwa mazoea" amesema 

Naye Daktari wa wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) ambaye pia ni mtafitll wa mamba Dkt. Iddi Lipende amesema mpaka sasa Serikali imejenga jumla ya vizimba 6 vya mfano nchi nzima ambapo vinne kati ya hivyo vimejengwa katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kwa lengo la kupunguza athari za wanyamapori aina ya mamba. 

Vizimba hivi vimekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi hususani akina mama na watoto ambao, tafiti zinaonyesha kuwa ndio waathirika wakubwa wa mashambulizi ya mamba 

Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikitenga fedha za ujenzi wa Vizimba vya mfano kupitia Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF) na TAWA na wataalamu kutoka TAWIRI.

Wananchi wa Kijiji cha Nyakaliro kilichopo Halmashauri ya Buchosa wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Vizimba hivyo na kukiri kuwa vinawasaidia kuwahakikishia usalama na kuendelea na shughuli zao za kijamii kama kawaida.

"Mwanzoni tulikuwa na shida kubwa sana ya mamba watu walikuwa wanakamatwa watoto wanakufa kwa ajili ya mamba lakini kutokana na hiki kizimba sasa hivi naona mamba hawatakuwepo kabisa, tunawashukuru TAWA, TAWIRI na Wizara ya Maliasili kwa ujumla kwa kutujengea hiki kizimba amesema Felista Majaliwa Mkazi wa Kijiji cha Nyakaliro.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema kufuatia changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake imekuwa ikifanya jitahada za makusudi katika kuhakikisha inaokoa maisha ya wananchi.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2024 TAWA ilifanya jumla ya mikutano 84 ya kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu mbalimbali za kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko katika vijiji 44 na shule 40 ambapo jumla ya watu 53,639 walifikiwa na elimu hiyo. 

No comments:

Post a Comment