Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Mheshimiwa Bacar Salim ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa kupitia Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro uliomalizika hivi karibuni, Serikali ya Tanzania imeharakisha mazungumzo na kuingia makubaliano katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa Kidiplomasia.
Mheshimiwa Balozi Salim amesema haya leo wakati Ujumbe wa Comoro uliokuja hapa nchini kushiriki mkutano huo, ulipotembelea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na kukutana na kuzungumza na Dkt. Jacob G. Nduye Kaimu Mkurugenzi kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa zilizopo katika masuala ya kitaaluma kati ya Tanzania na Comoro.
“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuingia makubaliano yenye faida kwa pande zote mbili, mazungumzo yalienda haraka na uamuzi ukafikiwa mapema tunashukuru. Comoro na Tanzania tuna Undugu, Ujirani, Urafiki na Wacomoro wanapokuja Tanzania wapo nyumbani” amesema Mheshimiwa Balozi Salim.
Akizungumza wakati wa majadiliano, Kaimu Mkurugenzi Dkt Jacob G. Nduye ameushukuru ujumbe kutoka Comoro kwa kuamua kukitembelea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na amesema Kituo kinatoa mafunzo ya muda mfupi, muda mrefu na programu maalum katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Stadi za Stratejia, Lugha mbalimbali na kufanya utafiti.
Kwa upande wa fursa, Dkt. Jacob G. Nduye amesema kupitia majadiliano yaliyofanyika miongoni mwa fursa zilizopo kwa pande zote mbili kati ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Vyuo vya Elimu ya juu vilivyopo nchini Comoro ni kubadilishana wataalam, programu za mafunzo na lugha mbalimbali.
Ujumbe wa Comoro umeongozwa na Bw. Abdou Nassir Madi, Mkurugenzi Mkuu wa Biashara na Waziri wa zamani wa Uchumi wa Comoro; Bw. Faicoil Mohamed Djitihadi, Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa na Sheria na Bw. Hassane Oumair, Mtaalam wa Sheria, Idara ya Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Comoro.
No comments:
Post a Comment