Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wapili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Water.Org, Eng. Francis Musinguzi kwa pamoja wakionesha mikataba ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai 2024. Wangeni pichani ni wanasheria wa Benki ya CRDB na Shirika la Water.Org.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wapili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Water.Org, Eng. Francis Musinguzi wakibadilishana mikataba ya ushirikiano ushirikiano katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam tarehe 18 Julai 2024.
Dar es Salaam. Tarehe 18 Julai 2024: Benki ya CRDB imesaini mkataba wa makubaliano na shirika la Water.Org Afrika unaolenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na mazingira safi katika maeneo mbalimbali nchini. Ushirikiano huu unaonyesha dhamira ya Benki ya CRDB katika kuchangia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki hiyo, Bruce Mwile alisema kuwa makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Benki ya CRDB ambayo inaelekeza katika kutoa suluhisho bunifu kwa jamii ili kukuza ustawi wa wadau wake.
"Tunajivunia kuona tunaendelea kuishi azma yetu ya kuchochea ustawi wa jamii kupitia ubia wa kimkakati na wenzetu wa Water.Org. Nizishukuru timu zetu za kitaalamu ambazo zimefanya kazi kubwa hadi kufikia hatua hii ambayo inatoa fursa kwa jamii kunufaika na uwezeshaji katika sekta ya maji na usafi," alisema Mkurugenzi huyo.
Mwile amesema ushirikiano huo utawezesha miradi ya sekta ya maji pamoja na usafi wa mazingira kwa kutumia fedha zitakazotengwa katika maeneo mbalimbali. Miongoni ya maeneo hayo ni pamoja na utafiti na ufadhili wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, mikopo ya miundombinu ya maji na usafi.
Benki hiyo intarajia pia kutoa mikopo midogo kwa watu binafsi, wajasiriamali, biashara, na taasisi kwa ajili ya kufunga miundombinu ya maji ya nyumbani, vifaa vya matumizi ya maji kwa ufanisi, na ujenzi wa vyoo na matangi ya maji safi na maji taka.
Aidha alisema mikopo hiyo pia itaelekezwa kwa sekta ya kilimo hususani kwa wakulima wanaotumia mifumo ya umwagiliaji yenye matumizi ya maji kwa ufanisi. “Ushirikiano huu pia utawezesha uanzishwaji wa huduma za bima zitakazotoa ulinzi dhidi ya majanga yanayoathiri miundombinu ya maji.” aliongezea Mwile.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Water.Org, Injinia Francis Musinguzi amesema kuwa ushirikiano huu unalenga kwenye kuboresha maisha ya jamii inayotuzunguka pamoja na hayo aliongezea kuwa utawezesha ufadhili wa tafiti za hatifungani za maji na usafi wa mazingira, pamoja na kuanzishwa kwa miradi endelevu ya maji na usafi.
“Ushirikiano huu pia utawezesha ufadhili wa tafiti za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufadhili miradi mikubwa ya usambazaji maji na usafi, pamoja na ufadhili wa bunifu za usimamizi wa maji kwa teknolojia,” alisema Injinia Musingizi.
Katika eneo la elimu na uhamasishaji, Benki ya CRDB na Water.Org watashirikiana kufadhili kampeni za elimu na uhamasishaji kuhusu umuhimu wa usafi ili kuzuia magonjwa, kupitia taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo imejikita zaidi katika kutoa elimu kwa jamii na kutoa mitaji wezeshi kwa wajasiriamali wanawake na vijana.
Makaubaliano ambayo Benki ya CRDB imeingia na Water.Org ni mwendelezo dhamira yake ya kuchangia ufikiaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan Lengo namba 6, 'Maji Safi na Usafi wa Mazingira'.
No comments:
Post a Comment