KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTAALAM UNAOTOLEWA KITUO CHA MFANO LWAMGASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 16, 2026

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTAALAM UNAOTOLEWA KITUO CHA MFANO LWAMGASA


Na Mwandishi Wetu - Lwamgasa , Geita


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wameonyesha kuridhishwa uchimbaji wa kisasa na utaalam wa mafunzo yanayotolewa katika Kituo cha Mfano cha Lwamgasa kilichopo mkoani Geita.

Hayo yamebainika leo Machi 16, 2026 na Mwenyekiti wa wakati ziara ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini lenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya kimkakati na utoaji wa huduma za kiufundi kwa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu nchini.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa kituo , Mgalu amekisifu kituo hicho kwa kuwa mhimili muhimu katika kuleta mapinduzi ya teknolojia kutoka uchimbaji wa mazoea kwenda kwenye uchimbaji wa kisasa na wenye tija.

Mgalu amesema kuwa utaalam unaotolewa hapo unawasaidia wachimbaji wadogo kuongeza kiwango cha dhahabu wanayopata (recovery) kutoka asilimia 30 hadi kufikia zaidi ya asilimia 80.

"Tumejionea namna kituo hiki kinavyowasaidia wachimbaji wetu wadogo kupata msaada wa kijiolojia, uchoraji wa ramani za migodi, na mbinu salama za uchenjuaji bila kutumia zebaki. Huu ni ushindi mkubwa kwa mazingira na uchumi wa mchimbaji mmoja mmoja," amesema Mgalu

Mgalu ameongeza kuwa, kituo cha Mfano cha Lwamgasa kimekuwa kielelezo cha namna Serikali, kupitia Wizara ya Madini na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), inavyowezesha wachimbaji wadogo kupata vifaa vya kisasa na utaalamu wa kimaabara kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde ameishukuru Kamati ya Bunge inayosimamia miradi ya Sekta ya Madini kwa ushauri mzuri uliotolewa ambao unaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hususan katika uchimbaji na uchenjuaji madini.

Waziri Mavunde , ameongeza kuwa Sekta ya Madini inasimamia miradi ya kimkakati ambayo lengo lake kubwa ni kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo ikiwemo uchorongaji wa miamba na uchenjuaji bora kupitia teknolojia ya CIP. Aidha Mavunde ameahidi kuwa maoni yote yalitolewa na wajumbe wa kamati yatafanyiwa kazi.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa STAMICO Deusdedith Magala ameifahamisha Kamati kuwa kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya vitendo kwa vikundi mbalimbali vya wachimbaji kutoka mikoa ya Geita, Mwanza, na Shinyanga, jambo linalopunguza ajali migodini na kuongeza mapato ya serikali kupitia mrahaba.

Kamati hiyo imehitimisha ziara yake kwa kuitaka Wizara ya Madini kuongeza vituo vingine kama hicho katika kanda nyingine za madini nchini ili kuwafikia wachimbaji wengi zaidi na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.

Katika ziara hiyo Mhe.Mavunde aliambatana na Naibu Waziri wa Madini na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Madini.

No comments:

Post a Comment