WAZIRI MKUU AAGIZA UCHUNGUZI WA UNUNUZI WA MABATI 4,000 MABOVU KATIKA UJENZI WA SHULE YA KATAVI BOYS - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 16, 2026

WAZIRI MKUU AAGIZA UCHUNGUZI WA UNUNUZI WA MABATI 4,000 MABOVU KATIKA UJENZI WA SHULE YA KATAVI BOYS


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu ununuzi wa mabati yasiyokidhi viwango yaliyokusudiwa kutumika katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Katavi (Katavi Boys), hatua iliyosababisha Serikali kutoa fedha mara mbili kwa ajili ya ununuzi wa mabati.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Machi 16, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Maridadi, Mpanda Mjini mkoani Katavi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alihoji mchakato wa ununuzi wa mabati takribani 4,000 yenye thamani ya karibu shilingi milioni 198, ambayo yalibainika kuwa hayakukidhi viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

“Takribani milioni 200 imenunua mabati yasiyofaa. Nani aliagiza haya mabati? Kwa nini Serikali itoe fedha mara mbili kwa jambo hilo?” alihoji Waziri Mkuu.

Baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumburi, Waziri Mkuu alieleza kutoridhishwa na namna suala hilo lilivyoshughulikiwa na kuagiza wahusika wote kuwajibishwa.

“Mkandarasi ambaye ameleta mabati yasiyofaa na watumishi wote waliohusika wakamatwe mpaka fedha ya Serikali irudi, na wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Sipha Nkusi Mwanjala, kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ushiriki wa kila mtu katika mchakato wa manunuzi hayo.

 “Kamanda wa TAKUKURU chunguza wote, kila mmoja tuone ushiriki wake. Hatuwezi tukaanza kubembeleza watu kwenye fedha ya umma,” alisema.

Vilevile, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi (RPC), Kaster Ngonyani, kuhakikisha mkandarasi aliyesambaza mabati hayo pamoja na watumishi wote waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Mkandarasi (Mzabuni) aliyesambaza mabati hayo ni kampuni ya Resa Roofers Limited ya jijini Mwanza inayomilikiwa na Bw. Samwel Richard.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alielekeza kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa mbolea katika Chama cha Ushirika wa Mazao (AMCOS) cha Ilangu kilichopo Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi.

Taarifa zinaonesha kuwa mbolea aina ya NPK 10:18:24 yenye thamani ya dola za Marekani 33,000 (sawa na takribani shilingi milioni 91) ilihusishwa katika ubadhirifu huo, huku baadhi ya watuhumiwa wakidaiwa kurejesha fedha lakini bado wakiendelea kushika nafasi za uongozi wakati kesi ikiendelea mahakamani.

 “Nimeambiwa hawa walioiba mbolea wamerudisha fedha hizo na kesi iko mahakamani, lakini bado wanaendelea kuwa viongozi. Kwa nini watu walioiba na imethibitika mmewaacha waendelee kuwa ofisini?” alihoji.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu alimtaka Waziri anayehusika kusimamia sekta hiyo kuhakikisha watuhumiwa hao wanaondolewa mara moja katika nafasi zao za uongozi wakati kesi yao ikiendelea mahakamani.

 “Wezi wanakaaje ofisini? Mnaachaje watu walioiba waendelee kuwa ofisini? Waondoeni haraka,” alisema.

Aidha, Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa kurejeshwa kwa fedha pekee hakufuti kosa lililofanyika, na kwamba wahusika wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.

 “Watanzania wanalipa kodi si kwa sababu wana fedha nyingi, wanajibana ili maendeleo yafanyike. Hatuwezi kukubali fedha ya umma ipotee kwa uzembe au kwa makusudi,” alisema.

No comments:

Post a Comment