Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wa Polisi (SACP) Theopista Mallya amewataka wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Huruma kutokujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi angali bado ni wanafunzi ili kujiepusha na mimba za utotoni pamoja na magonjwa ya kuambukiza.
Ameyasema hayo July 13, 2024 wakati akitoa elimu ya ukatili kwa wanafunzi wa shule hiyo ambapo amesema hakuna makubaliano ya mahusiano ya kufanya mapenzi na mtu ambaye ana umri chini ya miaka 18, kufanya hivyo ni makosa na adhabu yake ni jela miaka 30 au kifungo cha maisha.
Kamanda Mallya amekemea vitendo vya usagaji, ushoga, ulawiti pamoja ubakaji ambapo amewataka wanafunzi hao kuwahamasisha wazazi pindi wanapokuwa nyumbani kuchukia vitendo hivyo na kuvitolea taarifa kwa Jeshi la Polisi ili viweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Aidha Mallya amesema kazi ya mwanafunzi iliyo mleta shuleni ni kusoma na si vinginevyo hivyo wasipende zawadi ndogo ndogo zitakazo sababisha kukwamisha ndoto zao za kusoma kwa kubeba ujauzito na kupata magonjwa ya zinaa.
Katika hatua nyengine Kamanda Mallya amewataka wanafunzi hao kuishi katika maadili mema na kuchukia vitendo vya rushwa kuanzia sasa na kipindi watakachokua na madaraka kwani vitabu vya dini navyo vinapinga rushwa akinukuu kitabu cha Zaburi 15:5.
Toka Dawati la Habari Polisi Dodoma
No comments:
Post a Comment