![]() |
Mkulima Tambala Jefwa aliachwa na jicho moja baada ya kushambuliwa |
BBC Africa Eye inachunguza tuhuma za kushtua za wazee wanaotuhumiwa kwa uchawi kisha kuuawa katika pwani ya Kilifi nchini Kenya, ili kugundua sababu za kweli za mauaji hayo.
Tambala Jefwa mwenye umri wa miaka sabini na nne anatumia jicho moja lililosalia kuona, huku mkewe, Sidi, akilivua shati lake taratibu.
"Walimchoma kwa kisu na kumvuta," anasema, akionyesha kovu refu lililofika kwenye mfupa wa shingo.
Mke wake anatuonyesha kovu jingine la Jefwa, "ilibidi wavute ngozi ya kichwa na kuishona pamoja."
Jefwa anatuhumiwa kuwa mchawi na ameshambuliwa mara mbili nyumbani kwake, kilomita 80 (maili 50) kutoka pwani ya mji wa Malindi. Shambulio la kwanza lilimwacha bila jicho. Na la pili karibu aage dunia.
Wanandoa hao wanamiliki zaidi ya ekari 30 za ardhi, wanalima mahindi na kufuga kuku.
Kumekuwa na mzozo na wanafamilia kuhusu mipaka. Wanaamini hiyo ndiyo sababu hasa ya Jefwa kushambuliwa, si kwamba watu wanaamini kweli ni mchawi.
“Niliachwa nife. Nilipoteza damu nyingi sana. Sijui ni kwa nini walinivamia, lakini itakuwa inahusu ardhi tu,” anasema Jefwa.
![]() |
Sidi Jefwa akionyesha makovu ya kushambuliwa ya mumewe |
Imani za uchawi na ushirikina ni imani maarufu katika nchi nyingi.
Lakini katika maeneo ya Kenya, Malawi, Tanzania na Afrika Kusini, inaweza kutumika kama kisingizio cha kuua wazee ili kuchukua ardhi yao.
Ripoti iitwayo, The Aged, on Edge, ya shirika la kutetea haki za binadamu nchini Kenya, Haki Yetu, inasema mzee mmoja huuawa katika ufuo wa Kilifi kila wiki kwa tuhuma za uchawi.
Afisa mipango wa shirika hilo, Julius Wanyama, anasema familia nyingi zinaamini, ni mmoja wa wana familia anayeamuru mauaji hayo.
"Wanatumia neno uchawi kuhalalisha mauji kwa sababu watapata uungwaji mkono wa watu. Na watu watasema: ‘Kama alikuwa mchawi, ni vizuri umemuua.”
Ni watu wachache katika eneo hili wenye hati miliki za ardhi zao. Wanategemea kuirithisha ardhi hiyo, kwa wana familia.
Wanyama anasema mauaji saba kati ya kumi ya wazee, ni kwa sababu ya umiliki wa ardhi na urithi kuwa mikononi mwao.
"Kihistoria watu hapa Kilifi hawana hati za ardhi. Hati pekee walizo nazo ni simulizi kutoka kwa wazee hawa.
Ndiyo maana wengi wao wanauawa, kwa sababu mara tu unapowaua, umeondoa kikwazo,” anasema Wanyama.
(Katana Chara sasa anaishi katika makazi ya wazee kwani hawezi tena kujihudumia.
Takribani mwendo wa saa moja kwa gari kutoka ardhi ya familia ya Jefwa kuna kituo cha uokoaji wa wazee kinachoendeshwa na shirika la hisani, Chama cha Wilaya ya Malindi.
Ni nyumbani kwa takriban wazee 30 ambao wameshambuliwa na hawawezi kurejea katika ardhi yao wenyewe.
![]() |
Katana Chara mwenye umri wa miaka sitini na tatu, ambaye anaonekana ni mzee zaidi ya umri wake, amekuwa hapa kwa takribani miezi 12. |
Ilibidi ahamie kituoni hapa baada ya kushambuliwa kwa panga katika chumba chake cha kulala Aprili 2023. Mkono mmoja ulikatwa kwenye kifundo cha mkono, mwingine ulikatwa juu ya kiwiko.
Hawezi tena kufanya kazi na anahitaji usaidizi kwa kazi za kawaida tu, kama kula, kuoga au kuvaa nguo.
"Ninamfahamu mtu aliyenikata mikono, lakini hatujawahi kukutana ana kwa ana tangu wakati huo," anasema.
Chara alituhumiwa kuwa mchawi kutokana na kifo cha mtoto wa mtu mwingine, lakini anaamini sababu hasa ya yeye kushambuliwa ni shamba lake la ekari sita.
“Sina uhusiano wowote na uchawi. Nina kipande kimoja cha ardhi na kiko karibu na bahari. Ni sehemu kubwa ya ardhi.”
Wanafamilia wa Chara walihojiwa kuhusu shambulio hilo lakini hakuna mtu aliyewahi kufunguliwa mashtaka. Mwanaharakati Wanyama amekuwa akijaribu kumtafutia haki.
“Ni watu wachache sana wameshtakiwa kwa tuhuma za mauaji ya wazee. Na ndio maana, naamini watu wanaohusika kuua wanajiona wako huru.”
Baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa, BBC Africa Eye ilifanikiwa kukutana na muuaji wa zamani, anayedai kuwaua takribani watu 20.
Anasema kiwango cha chini alicholipwa kwa kila mauaji kilikuwa ni shilingi za Kenya 50,000 – karibu dola za kimarekani 400.
“Mtu akiua mzee ujue familia yake ililipia. Ni lazima iwe familia yake,” aliambia BBC Africa Eye.
Akieleza kwanini anafikiria ni sawa kuchukua uhai wa mtu, anajibu: “Huenda nimefanya jambo baya kwa sababu nilipewa kazi hiyo na ni mimi ndiye niliyeua, lakini kwa mujibu wa sheria, kulingana na Mungu, mtu aliyenituma ndiye mwenye hatia.”
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya iliwasilisha hati kwa Umoja wa Mataifa Februari 2023 ikisema: “Uchomaji moto watu wanaotuhumiwa kwa uchawi, mauaji, na mashambulizi ya kimwili yameenea katika maeneo kama vile Kisii magharibi mwa Kenya na kaunti ya Kilifi katika pwani ya Kenya.”
Inaendelea kusema wanafamilia vijana wanaotaka kupata ardhi ya familia ni sababu kuu inayochochea mauaji hayo. Inasema mashambulizi na mauaji yaliongezeka kipindi cha ukame na njaa wakati vyanzo vya mapato vikiwa haba.
Wanyama anasema mauaji yanayotumia shutuma za uchawi kuhalalisha unyakuzi wa ardhi yamekuwa "janga la kitaifa"
“Lilianza kama suala la mkoa, lakini sasa limezidi. Tusipolishughulikia, tutapoteza kumbukumbu zetu za wazee."
![]() |
Jefwas wanaamini kuwa wanafamilia ndio waliohusika na mashambulizi dhidi ya mumewe |
Katika tamaduni za Kiafrika, wazee wanaheshimiwa kwa hekima na ujuzi wao.
Kilifi ni kinyume chake. Wazee wanaogopa kushambuliwa, wengi hupaka nywele zao rangi kama jaribio la kutaka waonekane bado vijana.
Ni nadra kwa mtu wa mkoa huu kunusurika baada ya kutuhumiwa kwa uchawi.
Ingawa Chara yuko salama sasa anaishi katika kituo cha uokoaji cha wazee, kwa Jefwa kuna hofu kwamba yeyote aliyejaribu kumuua atarudi tena.
No comments:
Post a Comment