LUGHA YA KALE YA KIAFRIKA ILIYO HATARINI KUTOWEKA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 8, 2024

LUGHA YA KALE YA KIAFRIKA ILIYO HATARINI KUTOWEKA.

Watu wa Chabu wanaishi Kusini-Magharibi mwa Ethiopia.

Ndani kabisa ya msitu wa Shekka, kusini-magharibi mwa Ethiopia, lugha ya kale ya Kiafrika inakabiliwa na hatari ya kutoweka.


Inajulikana kama Chabu, inazungumzwa na watu wa Chabu, jamii iliyoenea kusini magharibi mwa Ethiopia.


Idadi ya wazungumzaji wake inaelezwa kupungua hadi 700 kutoka 1000, kulingana na watafiti.


Dkt. Kibebe Tsehay, mwanaisimu katika idara ya lugha ya Kiamhari ya Chuo Kikuu cha Debre Berhan cha Ethiopia ametumia miaka kadhaa kutafiti lugha hiyo.


Akielezea kupungua kwa wazungumzaji wa Kichabu, anasema, “imekuwa moja ya changamoto kubwa, ambayo nakabiliana nayo katika kuandika lugha ya kale.”


"Tumefanya sensa ya nyumba kwa nyumba ili kujua idadi ya watu wanaozungumza Kichabu. Kuna wazungumzaji wa Kichabu wapatao 740 tu waliosalia," kulingana na hesabu zake.


Watu wa Chabu ni mojawapo ya jami ya wachache nchini Ethiopia. Wachabu na lugha yao hujulikana kwa majina mawili tofauti Mikeyir na Shabo na jamii iliyo karibu nao.


Watu wa Chabu kihistoria ni wawindaji na wafugaji nyuki, wanaishi katika famili ndogo ndogo na mara kwa mara hubadilisha eneo lao la kuishi.


Katika miaka ya hivi karibuni, mashamba ya kahawa na maendeleo mengine ya kibiashara yameingilia maeneo yao ya kuishi, na kuwalazimisha kutoka kwenye misitu, hadi vijijini.


Leo hii Wachabu wengi wanaoishi katika msitu wa Shekka wanawinda kwa kiasi kidogo sana, lakini bado wanaendelea kuishi kwa kuwinda na kilimo cha kujikimu.


Wachabu wameanza kulima mazao kama vile ndizi, kahawa, mahindi, mapapai na miwa.


"Watu wa Chabu waliishi kwa kutawanyika katika msitu, kwa njia ambayo iliendana na mahitaji yao. Lakini wameanza kuishi pamoja vijijini,” anasema Kibebe.


Walipokuwa wakikutana na watu wa Chabu, watafiti walibainisha kuwa jamii za jirani, hasa watu wa Majan na Shekkacho, walikuwa wakihamia karibu na maeneo ya Chabu kutafuta ardhi ya kulima. 


Ukaribu huu ulikuwa unaififisha zaidi lugha ya Chabu.


Watu wa Chabu kihistoria ni jamii ya wawindaji 


"Kinachofanya lugha ya Kichabu kuwa ya kipekee ni kwamba haijajumuishwa katika kundi lolote la lugha za Kiafrika," anaelezea Profesa Kibebe.


Lugha zinazozungumzwa nchini Ethiopia ni zile za kundi la Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, ziitwazo Afro-Asiatic na zile za kundi la katikati ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ziitwazo Nilo-Saharan.


Lugha nyingine zinazozungumzwa Afrika ni zile za kundi la Semitiki, Kikushi na Kiomotiki. Na kundi jingine ni Koishan na Niger-Congo.


Kibebe anaeleza, Kichabu hakijajumuishwa katika kundi lolote la makundi ya lugha zinazojulikana Afrika.


"Inadhaniwa huenda inatokana na kundi la lugha za kale sana za Kiafrika ambazo labda zimetoweka," anaongeza.


Iliripotiwa kwa mara ya kwanza kama lugha tofauti mwaka 1977 na mwanaisimu wa Marekani Marvin Lionel Bender, sarufi na sintaksia yake ilihifadhiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015. Na hadi leo, nyingi ya sarufi zake zimegubikwa na siri.


Katika luga ya Chabu, mpangilio wa maneno ya msingi huanza kama ‘mtenda – mtendwa – kitenzi.’ Ikiwa sentensi yako ni 'Mtu aliona mbwa' katika lugha ya Kichabu itakuwa ‘Mtu mbwa aliona.’


Watafiti wanaamini hiyo sio sifa pekee ya lugha hiyo.


Watu wa jamii ya Chabu wakicheza katika sherehe 


Kutokana na uhamiaji na mchanganyiko wa jamii mbalimbali, Kibebe anabainisha jambo muhimu, Wachabu wamelazimika kujifunza kuzungumza lugha nyingine, wakati jamii nyingine hazijalazimika kujifunza Kichabu. Anasema hii ndiyo sababu kuu inayochangia kutoweka kwa lugha hiyo.


Profesa Kibebe pia anabainisha katika utafiti wake, lugha ya Kichabu inazidi kuwa lugha ya pili ya kizazi kipya cha Wachabu, kiashiria cha kupungua hadhi ya lugha hiyo.


"Lugha yoyote inapopotea, urithi wake pia hupotea," ameiambia BBC.


"Lugha kwa jamii yoyote, ni hati ambayo ndani yake inashikilia mila, utamaduni, falsafa na maarifa ya zamani, hekima na desturi."


Hii inamaanisha kukipoteza Kichabu, itakuwa sawa na "kuchoma maktaba," anaongeza.


Kwa kuwa Kichabu ndiyo lugha pekee inayojulikana katika kundi lake la kipekee, ikiwa itatoweka kabisa, hasara yake itakuwa kubwa zadi.

No comments:

Post a Comment